Aliyekua Kocha Mkuu wa Namungo FC Honour Janza, Rasmi amejiunga na Klabu ya ZESCO United ya nchini kwao Zambia kama Mkurugenzi wa Ufundi.

Janza ambaye alikuwa Kocha wa muda wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ amefikia makubaliano na Uongozi wa ZESCO United, baada ya kukamilisha mazungumzo ya awali, ambayo yalimlazimu kuiacha Namungo FC na kurudi nyumbani kwao.

Janza ambaye pia aliwahi kuwa Kocha wa Mkuu wa Timu ya Taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’, amesaini mkataba wa miaka mitatu na wababe hao wa ligi kuu ya Zambia.

Akitangaza uteuzi huo, Mwenyekiti wa klabu hiyo Maxwell Saya alisema “Janza ni meneja mwenye sifa za juu na amefanya kazi katika kiwango cha juu kabisa cha soka la Afrika na anakuja na sifa kubwa”

“Tuna matumaini kwamba uzoefu wake mkubwa katika michezo utaimarisha maendeleo ya soka katika klabu,” Saya alisema.

Kuondoka kwa Kocha huyo kumetoa nafasi kwa Uongozi wa Namungo FC kufanya kazi na Kocha Mzawa Denis Kitambi, ambaye kwa mara ya kwanza alionekana katika Benchi la Ufundi wakati wa mchezo dhidi ya Young Africans uliopigwa juzi Jumatano (Decemba 07).

Janza alianza kuitumikia Namungo FC Januari mwaka huu, akichukua nafasi ya Kocha Kocha Hemed Morocco ambaye aliamua kuondoka kutokana na kikosi cha Namungo FC kukosa matokeo mazuri kwa wakati huo.

Janza alianza Kazi klabuni hapo akisaidiana na Kocha Mzawa Jamuhuri Kiwelu Julio.

Polisi yatoa huduma za matibabu kwa Wazee
Azam FC wafunguka Kally kuachwa tuzo ya Kocha Bora