Kampuni ya Star Times imeingia Mkataba wa miaka mitatu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya udhamini wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara wenye thamani ya Sh Milioni 900.

Mkurugenzi Mkuu wa Star Times, Lanfang Liao amesaini Mkataba huo mbele ya Waandishi wa Habari na Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi katika ukumbi wa mitano wa Kisenga uliopo jengo la LAPF Kijitonyama, Dar es Salaam.

Sasa Ligi Daraja la Kwanza ambayo ilianza wiki iliyopita, itakuwa inaonyeshwa moja kwa na katika chaneli za Star Times.

Akizungumza baada ya kusaini Mkataba, Malinzi amesema kwamba sasa ligi hiyo itaitwa Star Times First Division League (Ligi Daraja la Kwanza ya Star Times) na itashirikisha klabu 24 kutoka mikoa 16 ya Tanzania Bara na kwamba kila klabu itapata Sh. Milioni 15.

“Hii ni Ligi muhimu sana kwa sababu inatoa wachezaji ambao hupanda Daraja na kucheza Ligi Kuu, siyo ligi ya kubeza,” amesema Malinzi.

Malinzi ambaye ni Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga SC, amsema kwamba wiki ijayo pia watasaini mkataba na mdhamini mwingine kwa ajili ya Ligi hiyo.

Amesema baada ya kusaini Mkataba na mdhamini huyo wa pili, dau la jumla la udhamini wa Ligi Daraja la Kwanza litafikia Sh. Bilioni 1.35.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Star Times Lanfang Liao amesema kwamba huo ni mwanza tu, kuna makubwa zaidi yatakuja na lengo ni kutoa nafasi ya kutangaza vipaji vya wachezaji wa Tanzania nje ya nchi.

Mapema mwezi huu, Malinzi alisaini Mkataba wa udhamini wa Kombe la TFF na Azam TV- michuano ambayo ilikuwa imekufa sasa inarudi tena nchini.

Na hii ni mara ya kwanza kabisa katika historia ya Ligi Daraja la Kwanza kuwa na udhamini tangu ikiwa ndiyo ligi kubwa zaidi nchini kabla ya kuanzishwa kwa Ligi Kuu.

Sir Alex Ferguson: Moyes Alikuwa Sahihi Kwa Man Utd
Utafiti Wa 'TWAWEZA' Wampa Magufuli Ushindi Wa Kishindo Dhidi Ya Lowassa