Baada ya kikosi cha Azam FC kurejea nchini kikitokea Zambia kilipokua kimeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu na Michuano ya Kombe la Shirikisho, Uongozi wa klabu hiyo umetoa tathimini fupi ya kambi waliyoiweka nje ya nchi.

kikosi cha Azam FC kiliwasili jijini Dar es salaam jana Jumatatu (Septemba 06) Alfajiri, kikitokea mjini Ndola (Zambia), ambapo walikua wameweka kambi ya zaidi ya juma moja iliyokwenda sambamba na kucheza michezo ya kimataifa ya kirafiki.

Afisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabiti ‘Zaka Zakazi’, amesema kikosi kambi yao ilikua nzuri na wanashukuru benchi lao la ufundi chini ya Kocha George Lwandamina kutumia muda mfupi walioupata kutimiza Program waliokua wamejiwekea.

Hata hivyo Zaka Zakazi amesema licha ya kufanikiwa huko, kuna baadhi ya mambo hayakwenda sawa, na wameyachukua kama changamoto iliyowakwamisha kwa asilimia fulani, hasa upande wa kuwakosa baadhi ya wachezaji walioitwa kwenye timu zao za taifa.

Amesema walikuwa na wachezaji 19 pekee badala ya 29, jambo ambalo lilikwamisha maandalizi yao kwenda kama walivyotarajia.

“Kambi ilikuwa na mafanikio makubwa kwa kupata kile kinachohitajika kwa kucheza mechi za kirafiki, zimempa mwaga kocha Lwandamina (George) kuona mapungufu yake, lakini hakuweza kupata mazoezi ya kimbinu kwa sababu ya kuwapo kwa uchache wa wachezaji,” amesema Zaka.

Amesema wamerejea nchini kuendelea na mazoezi ya kawaida kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Horseed SC ya Somalia, kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Azam FC watacheza mchezo wa kwanza Jumamosi (septemba 11), katika Uwanja wa Azam Complex na mchezo wa marudiano utapigwa kwenye dimba la Uhuru jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma lijalo.

RC Makalla kusimamia maboresho mnada wa Pugu
TP Mazembe kuipima Simba SC