Vinara wa ligi kuu ya soka Tanzani bara Wekundu Wa Msimbazi Simba watafungua pazia la michuano ya kombe la Mapinduzi 2018 dhidi ya URA kutoka nchini Uganda, Januari 2 Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja mishale ya 2:15 usiku.

Simba watafungua michuano hiyo huku wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa fainali wa michuano hiyo mwanzoni mwa mwaka huu, kwa kufungwa bao moja kwa sifuri na Azam FC, jambo ambalo huenda likawapa chachu ya kutamani kurejea mafanikio hayo.

Kwa upande wa mabingwa wa soka Tanzani bara Young Africans wataanza kampeni ya kuuwani ubingwa wa michuano ya kombe la Mapinduzi 2018, kwa kucheza na JKU ya Zanzibar mnamo Januari 1 kwenye Uwanja wa Amaan, mchezo ambao utachezwa kuanzia 2:15 usiku.

Mabingwa watetezi wa michuano hiyo Azam FC, wataanza kempni ya kutetea ubingwa wao dhidi ya Jamhuri ya Pemba.

Ufunguzi rasmi wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2018 utafanyika Desemba 30, mwaka huu kwa michezo miwili Uwanja wa Amaan, ambapo Zimamoto watapapatuana na Mlandege Saa 10:15 jioni na baadaye JKU watapepetana na Shaba Saa 2:15 usiku.

Simba SC imepangwa Kundi A pamoja na Azam FC, Jamhuri, Taifa ya Jang’ombe na URA ya Uganda, wakati Young Africans imetupwa Kundi B pamoja na JKU, Mlandege, Zimamoto na Shaba.

Simba itamenyana na Azam FC Januari 6, ikitoka kukipiga na Taifa ya Jang’ombe Januari 4, kabla ya kumalizia michezo yake ya Kundi A Januari 8 dhidi ya Jamhuri.

Azam FC itacheza na Taifa ya Jang’ombe Januari 4 kuanzia Saa 10:15, kabla ya kumenyana na Simba na itahitimisha michezo yake ya kundi A kwa kuumana na URA Januari 8 Saa 10:15 jioni.

Baada ya mchezo dhidi ya JKU, Young Africans watarudi tena dimbani Januari 3 kwa mchezo dhidi ya Shaba, Januari 5 na Zimamoto kabla ya kukamilisha michezo ya Kundi B kwa kumenyana na Mlandege Janauri 7 Uwanja wa Amaan.

Nusu Fainali zinatarajiwa kuchezwa Januari 10 na Fainali itakuwa Januari 13, Uwanja wa Amaan kuanzia Saa 2:15 usiku.

Wachezaji TP Mazembe wajazwa noti
Angalia orodha ya wafungaji 10 bora Ligi Kuu Tanzania Bara