Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera, amedai kuwa wapinzani wake wamemzushia kauli ya kuagiza kurogwa kwa wananchi ili washiriki kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,kama ambavyo alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini.

Homera ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Katavi, ambapo amesema hiyo si mara ya kwanza kuzushiwa hivyo kwa watu ambao yeye mwenyewe amedai wanatokana na masuala ya kisiasa, bali alichokisema watu mbalimbali wakiwemo waganga wa jadi wanapaswa kufanya ibada ili uchaguzi uishe kwa amani.

“Najua wanaofanya hivyo ni wenzetu wale wa upande wa pili, kwakuwa huku Katavi nimewashika pabaya nawanyoosha kama rula, eti mimi nimewataka waganga kuwaroga watu, hawa wanaosema haya wamechanganyikiwa na hawajaanza leo wameshanizushia mambo mengi” amesema Mkuu wa Mkoa Juma Homera.

Aidha Homera ameongeza kuwa, “nikiwa Tunduru walipiga picha darasa bovu, wakasema DC Tunduru amesema shida ya Darasa sio tatizo, shida na kipaumbele chake ni kukifuta chama fulani cha upinzani, kwahiyo hata haya ya kunizushia nimewataka waganga wa jadi kuwaroga watu siyashangai”.

Kauli ya kutaka waganga wa jadi kuwaroga wananchi ili waweze kushiriki vyema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, zilianza kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii siku ya Oktoba 27, 2019.

Mbeya City yachanua ugenini, Alliance FC yabanwa nyumbani
Harmonize azidi kupasua anga na Uno, atua Kigali, Rwanda