Miili ya watu 20 waliopoteza maisha wakati wakikimbilia kukanyaga mafuta ya upako, yaliyomwagwa mlangoni na Mtume Boniface Mwamposa, wakati wa kongamano lake la kidini juzi Jumamosi, imeagwa leo Jumatatu, Februali 3, 2020 katika uwanja wa Majengo mkoani Moshi huku viongozi mbalimbali wakitoa salamu zao za rambirambi.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira, amesema kuwa tukio hilo limewaogopesha sana na kwamba ipo haja ya viongozi wa dini na Serikali wakakutana na kujadiliana.

“Jambo hili limetuogopesha, limetutia hofu lakini halijatuvunja moyo, liwe mwanzo wa kuimarisha mambo ya imani, viongozi wa dini mbalimbali tukutane na Serikali na mwisho tutawajulisha wananchi nini tumekubaliana” amesema RC Mghwira.

Ameongeza kuwa, “Kuna kichanga kabisa amepoteza maisha, tunao watoto wa miaka miwili, mitatu hadi 10 na wengine watu wazima, inauma sana sisi tulioshuhudia wakati maiti zinashushwa zilikuwa za moto inauma sana”

Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya, amesema kuwa licha ya kuwa wananchi kuwa na matatizo mengi viongozi wa dini wasitumie shida zao kama mitaji ya kujinenepesha wenyewe na hata maafa yakitokea basi wawe mstari wa mbele na si kukimbia.

“Ni kweli Wachungaji wananchi wetu wanateseka sana, wana mizigo mizito, wana shida kubwa sana, lakini msigeuze kuwa ni mitaji ya kuwasaidia watu huko mlipo, tendeni kama mnavyopaswa kutendewa na yakitokea haya msikimbie” amesema DC Sabaya. 

 

 

Mbunge aomba Serikali kuruhusu biashara ya bangi, Ndugai apigilia msumari
Video: Serikali yazindua muongozo wa matibabu ya Saratani