Wakurugenzi wa Halmashauri na Watendaji wa Wilaya zote za Mkoa wa Singida wameagizwa kufanya ziara kusikiliza kero za Wananchi na kuzipatia ufumbuzi badala ya kusubiri viongozi wa juu wa Serikali ya Mkoa kushughulikia kero hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge ameyasema hayo wakati wa kikao maalum cha kufanya majumuisho ya ziara yake aliyoifanya hivi karibuni katika wilaya zote za mkoa wa huo kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.

Amesema Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo lakini wananchi hawajui kinachoendelea kutokana na baadhi ya Viongozi ambao wanapaswa kuwaeleza kushindwa kuwafikia.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Bilinith Mahenge akiongea wakati wa kikao na Wakurugenzi na Watendaji wa Halmashauri zote za Mkoa wa Singida.

“Ni muhimu kufanya mikutano ya wananchi kusikiliza kero zao, wahamasisheni Madiwani, Makatibu Tarafa wafanye ziara, Mkoa wetu mwaka wa fedha uliopita tulipata Shilingi 230 bilioni ni wajibu wetu kama Viongozi kuzisimamia ili zilete tija katika maendeleo,” amesisitiza.

Aidha, Dkt. Mahenge ameongeza kuwa Wakuu wa Wilaya wamekuwa wakijitahidi kufanya ziara na kusikiliza kero za wananchi lakini changamoto ipo kwa watendaji wengine ambao wameshindwa kufanya hivyo na kusababisha kuibuka kwa kero zisizo na ulazima.

Akiongea mbele ya mkutano huo, Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuyafanyia kazi maelekezo yake kwa kushirikiana na Watendaji wa Halmashauri za Mkoa.

Baadhi ya Wakurugenzi wakiwa katika kikao na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Bilinith Mahenge.
Samia awapa pole waliovamiwa na Tembo
Nathaniel Chilambo anaswa Azam FC