Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mbeya, Albert Chalamila jana alifanya ukaguzi wa Fukwe za Ziwa Nyasa, hususan eneo la Matema wilayani Kyela kwa lengo la kubaini changamoto zinazokwamisha maendeleo ya Sekta ya Utalii katika eneo hilo.

Chalamila alieleza jinsi ambavyo barabara iliyojengwa kwa maagizo ya Rais John Magufuli kutoka Kyela Mjini hadi fukwe za Matema, iliyogharimu Sh. 65 bilioni ilivyoongeza fursa ya ukuaji wa utalii unaochochea maendeo ya kiuchumi katika eneo hilo.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais [John Pombe Magufuli] ametujengea barabara kutoka Matema hapa hadi Kyela Mjini, barabara ya gharama sana, ambayo imegharimu sio chini ya Sh. 65 bilioni kuwafikia wananchi wa Matema na wananchi wa Kyela kwa upana wake,” alisema Mkuu wa Mkoa.

Alisema kuwa kutokana na hatua hiyo, Mkoa huo sasa una jukumu la kuimarisha miundombinu ya barabara kwa ujumla, ili sehemu nyingi zaidi za fukwe ziweze kufikika kiurahisi.

“Kyela ina beach (fukwe) nzuri sana ambazo vina vyake vya maji sio virefu sana, lakini vilevile ni beach zenye asili ya mchanga. Na ukiangalia uchumi wa Zanzibar unategemea sana utalii wa kwenye fukwe. Kwahiyo hivi vitu viwili tukivileta hapa vitachochea uchumi na hata hawa wavuvi wote hizi beach zote zikijengwa watafaidika sana na uvuvi kwa sababu mlaji wa samaki atakuwa karibu,” alisema.

Aliongeza kuwa kwakuwa hivi sasa hali inaonesha kuwa uchumi umelala katika eneo hilo kutokana na ubovu wa miundombinu katika maeneo mengine, Jumatano atakutana na makandarasi na wadau wengine wa maendeo ili waweze kujadili jinsi ya kutatua changamoto hiyo.

“Hii ni kwa sababu ingawa barabara hii [ya Mheshimiwa Rais] imetumia Sh. 65 bilioni, bado vitu vilivyo ndani ya eneo hili haviakisi ule uwekezaji uliofanywa,” RC Chalamila alifafanua.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwaalika wananchi kwa ujumla kufanya utalii katika eneo hilo hata wakati huu ambapo bado wanaendelea kuhakikisha wanaboresha miundombinu mingine ili kuweza kufika kwa urahisi katika maeneo ya ndani zaidi.

Aprili 2019, Rais John Magufuli akiwa ziarani Wilayani Kyela mkoani Mbeya, alizindua ujenzi wa barabara hiyo ya lami yenye urefu wa Kilometa 39.1, kutoka Kikusya – Ipinda- Matema iliyogharimu Sh. 65 bilioni, kama inavyoonekana kwenye picha hapo chini akiwa na Mkuu wa Mkoa, Chalamila.

Dodoma FC kuanza mazoezi Al-Khamis

Jeshi la Polisi: Idris Sultan alijaribu kuharibu ushahidi

Ndayishimiye ahutubia taifa kwa mara ya kwanza kama Rais
Dodoma FC kuanza mazoezi Al-Khamis