Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amesema kuwa amewasamehe baadhi ya waandishi wa habari wa Mkoani humo ambapo amedai maazimio ambayo waliyatoa juu ya kumtaka aombe radhi, yalikuwa ni maamuzi ambayo hakuyafurahia.

Ameyasema hayo ikiwa ni siku chache baada ya waandishi wa habari mkoani humo, kumtaka kuomba radhi kwa kutoa orodha ya waandishi wa habari juu ya makundi ambayo yanahitaji kuwa na vitambulisho vya wajasiriamali wadogo.

“Walitoa tamko la siku 7, nikajiuliza RC unampa siku 7 unaelewa mamlaka yake, nadhani mliona kwenye vyombo vya habari waandishi na Mwenyekiti wao yuko hapa, nilikuwa safarini Mbeya naelekea Rukwa niliposoma nikawa nacheka nikasema ee Mungu wasamehe hawajui walitendalo.” amesema Hapi.

Aidha, amesema kuwa Mkuu wa Mkoa ni mwakilishi wa Rais hivyo wakimuona yeye sio pale alipo ni sawa na kwamba wamemuona Rais Magufuli hivyo hakuna mtu wa kumpa siku saba kwamba afanye kitu fulani.

Hata hivyo, Hapi ameongeza kuwa kumlazimisha yeye afanye jambo fulani ni kwamba kunatangaza vita na Rais hivyo amewataka waandishi wasifanye tena hivyo kwa kile alichokidai kuwa si jambo la busara sana.

Video: Bajeti ofisi ya CAG yafyekwa, Waisilamu wahimizwa kutenda mema , umoja
Wazee na Wajane wanufaika na hati miliki za kimila