Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu Raphael Muhuga amewaita wawekezaji wa usafiri wa anga kuwekeza kwenye Kiwanja cha Ndege cha Mpanda, kutokana na kuwa na miundombinu mizuri.

Amesema hayo kwa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), iliyofanya ziara kwenye kiwanja hicho, ambapo ameihakikishia wapo abiria wengi wa kutosha.

Pia, amesema kiwanja hicho kitaongeza pato la kila Mwananchi na taifa kwa ujumla kwa kuwa kipo kwenye Ukanda wa Kitalii  kwa kuwa na Hifadhi ya Taifa ya Katavi, karibu na Ziwa Tanganyika na Hifadhi za  Taifa za Gombe na Mahare zilizopo mkoa  wa jirani wa Kigoma.

Naye Mwenyekiti wa MAB, Mhandisi Prof. Ninatubu Lema amesema atahakikisha anawasiliana na uongozi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ili kujua mipango yao juu ya ndege zake zianze safari kwenye Kiwanja cha Mpanda.

Prof. Lema amesema endapo ndege nyingi zitatumia kiwanja hiki kitasaidia jamii za hapa kwa kiasi kikubwa ikiwemo kipato kukua na kukuza uchumi wa taifa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela amesema Mamlaka inaweka mambo mengi kimkakati katika kuhakikisha inatekeleza sera ya Uchumi wa Viwanda hasa katika sekta ya usafiri wa anga, ambapo ni pamoja na kuimarisha viwanja vya ndege nchini.

“Mnafahamu kuwa Serikali kupitia TAA imekuwa na utaratibu wa kuboresha viwanja vya ndege kwa maana ya miundombinu, mwaka jana tu peke yake Mhe. Rais amezindua miradi ya viwanja viwili vya Tabora na Bukoba, ambapo vimetengenezwa kwa viwango vya lami na vinaweza kuhudumia ndege kubwa zaidi,” amesema Mayongela.

Mayongela amesema kwa kushirikiana na Bodi wanatembelea viwanja ambavyo miradi imekamilika, iliyopo katika hatua mbalimbali za matengenezo na itakayoanza baadaye, ambapo ni katika viwanja Mtwara, Songwe, Songea, Musoma, Shinyanga, Sumbawanga na Iringa.

Amesema lengo la uimarishaji na kuboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege ni kurahisisha wawekezaji kufika maeneo mbalimbali ya nchi kwa haraka na urahisi, hivyo kwa wataalamu wanapotoka nje ya nchi na malighafi kusafirishwa kirahisi.

Mayongela amesema miundombinu bora ya viwanja vya ndege itasaidia ujio wa wataalam wengi wa shughuli mbalimbali, na kupunguza muda mrefu wa kukaa kwenye mabasi ya abiria kwa wananchi na wafanyabiashara mbalimbali.

Pia amesema kukamilika kwa miradi mbalimbali ya viwanja vya ndege kutatoa fursa za ajira kwa wananchi wengi, na kuongeza pato la taifa, pia viwanja vinachochea ukuaji wa sekta nyingine ikiwemo ya utalii, ambapo kwa mkoa wa Katavi watalii wengi wanaweza kutembelea Hifadhi ya Katavi na wagonjwa wataweza kuwahi matibabu kwenye hospitali kubwa.

Amesema wito wake wananchi watumie fursa za kuwekeza kwenye kiwanja cha ndege cha Mpanda.

Naye Meneja wa Kiwanja cha ndege cha Mpanda, Seneth Lyatuu amesema katika taarifa yake kuwa kiwanja hiki kilianzishwa mwaka 1954 kikiwa chini ya Kampuni binafsi ya Uchimbaji wa Madini ya Urwila na kipo umbali wa Kilometa mbili (2) Kaskazini Mashariki mwa Mji wa Mpanda lakini baada ya Uhuru kilikabidhiwa kwa Serikali na mwaka 2008 kurefushwa kwa njia ya kutua na kuruka ndege kwa kiwango cha lami kutoka urefu wa mita 1500 na upana wa mita 30 hadi kufikia urefu wa mita 2000 kwa upana wa mita 30.

Lyatuu amesema pia eneo la maegesho ya ndege lilikarabatiwa na sasa linauwezo wa kuegesha ndege mbili aina ya ATR 42, au ndege ndogo aina Cesna 208 zipatazo nane (8) kwa wakati mmoja.

“Hapa Kiwanjani tunaendelea kutoa huduma bora kwa abiria, mizigo na ndege kwa kuzingatia miongozo ya Usalama kwa kufanya ukaguzi wa mizigo, uegeshaji salama wa ndege, kuboresha mazingira ya kiwanja,” amesema Lyatuu.

Pia, MAB imefanya ziara kwenye viwanja vya ndege vya Songwe, Njombe na Iringa.

Video: Matukio 11 yatikisa nusu mwaka, Vigogo wapigana vikumbo majimboni uchaguzi 2020,
Makonda aweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya Africana Kinzudi