Majeruhi mwingine wa ajali ya moto uliozuka baada ya lori la mafuta lililoanguka katika eneo la Msamvu mjini Morogoro kulipuka, amefariki dunia leo asubuhi na kusababisha idadi ya waliopoteza maisha kuwa 76.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Stephen Kebwe amewaambia waandishi wa habari kuwa hadi sasa majeruhi 38 wamefikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam na 16 wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa huo.

Aidha, ameeleza kuwa kati ya miili nane iliyokuwa inasubiri kutambuliwa, sita imepata ndugu na utaratibu unaendelea kwa miili mingine miwili.

Jumapili, Agosti 11, 2019 miili ya wahanga wengi zaidi wa ajali hiyo ilizikwa katika makaburi ya Kola Hill mjini humo ambapo baadhi ilikuwa imeharibika kufikia hatua ya kutotambulika.

Ajali hiyo ya moto ilitokea Jumamosi, Agosti 10, 2019 ambapo baadhi ya waathirika walikuwa wanajaribu kuchota mafuta kutoka kwenye lori lililoanguka.

Akizungumza na Dar24, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alisema kuwa wananchi wanapaswa kuwa wamejifunza kupitia matukio kama hayo ambayo yamewahi kutokea katika mkoa wa Mbeya.

“Tukio lililotokea Mbeya lilikuwa ni fundisho zuri tu la kutosha kwa Watanzania, kwa tukio hili ambalo linafanana na lile la Mbeya. Kwa hiyo mafunzo yapo mengi, yale ambayo ni ya kawaida yanayojirudia na mengine mapya ambayo tunapaswa kujifunza kwayo,” Waziri Mhagama aliiambia Dar24.

Aliongeza kuwa Serikali inapaswa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wake kuhusu kuchukua tahadhari na kutambua maeneo pamoja na matukio hatarishi.

“Lakini kwetu sisi kama Serikali tunapaswa kuendelea kuelimisha Wananchi, kitu ambacho kinaendelea kufanyika; na pia kuweza kuangalia utendaji kazi wa vyombo vyetu mbalimbali katika kusimamia matukio haya ambayo yanatokea mara nyingi barabarani,” aliongeza.

Serikali yaipongeza timu ya Tanzanite U20
Dkt. Bashiru Ally atoa msaada wa Mbuzi