Katika kuhakikisha kuwa wananchi wanajikwamua katika wimbi la umaskini, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,  Anthony Mtaka amesema kuwa Mkoa huo unahitaji ushirika imara na wa kisasa unaolenga kuwafikisha wananchi katika Uchumi wa kati.

Amesema  hayo wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa wa Simiyu uliofanyika Mjini Bariadi, tukio ambalo limeshirikisha viongozi Serikali na watalaam mbalimbali ngazi ya Mkoa na Wilaya, viongozi wa vyama vya ushirika, Tume ya maendeleo ya Ushirika  na wadau  mbalimbali wa ushirika.

” Sisi kama mkoa tuko tayari  kwa yale ambayo  ninyi wenzetu wa Tume ya Ushirika mnadhani kupitia hayo tutakuwa na ushirika imara na utakaoendeshwa kisasa, tuko tayari hata kwa kuwatoa watu wetu kujifunza katika vyama vya ushirika vilivyofanikiwa ushirika wa Tanzania ukiamua Uchumi wa kati inawezekana,”amesema Mtaka.

Amesema kuwa wananchi wakielimishwa na kukubali kuungana katika vyama ushirika wanaweza kuondokana na Umaskini, hivyo amesisitiza uwepo wa ushirika imara wenye matokeo chanya katika maeneo muhimu ya uzalishaji, ili hata mikoa mingine ijifunze kutoka Simiyu.

Aidha, Mtaka amesema  Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) imekubali kufanya kazi na Mkoa wa Simiyu kwa kuviwezesha vyama vya ushirika na  vikundi vilivyosajiliwa kisheria kwa kuwajengea uwezo wanachama na kuwapa mikopo kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali, hivyo vyama vya ushirika vinapaswa kuchangamkia fursa hiyo.

 

Kwa Upande wake Kaimu Naibu Mrajis kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Collins Nyakunga amemshukuru Mkuu  wa Mkoa wa Simiyu kwa kuonyesha nia ya kuimarisha ushirika katika mkoa huo na kuona kuwa kupitia ushirika wananchi wanyonge wanaweza kutatua matatizo yao ya kiuchumi na Kijamii.

Hata hivyo, Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Simiyu, Mathias Shineneko amesema kuwa Mkoa huo umejiwekea mkakati wa kuhakikisha vyama vya ushirika vinajielekeza katika kuweka taratibu za kuongeza  na kuimarisha mitaji, hisa na akiba ili kujiimarisha kiuchumi.

TRA yaidai Acacia kodi ya Trilioni 424, ni bajeti ya miaka 13
Video: Haijawahi kutokea, Werema afunguka kauli ya Tumbili