Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amezindua rasmi kambi ya kitaaluma kwa Wanafunzi wa Kidato cha sita kwa mwaka 2019 yenye wanafunzi 1166 na kuagiza taa zisizimwe usiku ili wanafunzi waweze kupata nafasi ya kujisomea zaidi.

Ametoa agizo hilo, wakati akizindua kambi hiyo kwa wanafunzi 1166 wa kidato cha sita na walimu mahiri 34 kutoka shule 12 za mkoa wa Simiyu, inayofanyika katika shule ya sekondari ya  wasichana ya Maswa.

Amesema ili mkoa wa SIMIYU uweze kushindana kiuchumi unapaswa kufanya mageuzi makubwa ya kielimu, hivyo elimu ni kiupaumbele cha mkoa ambapo ameagiza katika kipindi chote cha kambi wanafunzi waruhusiwe kusoma bila kuzimiwa taa darasani.

Aidha, amewahakikishia wanafunzi na walimu upatikanaji wa mahitaji yote muhimu wawapo kambini, ikiwa ni pamoja na ulinzi na usalama, upatikanaji wa chakula, maji, umeme, mahitaji mengine na kueleza kuwa tayari viti vipatavyo 1000 vimeshanunuliwa kwa ajili ya kambi hiyo.

“Ofisi yangu itatoa zawadi ya shilingi milioni tatu kwa mwanafunzi atakayepata ‘division one ya point tatu’ atakayepata ‘division one ya point 4 na 5’ atapata shilingi laki tano, shule itakayokuwa katika kumi bora Kitaifa itapata shilingi milioni tano,”amesema RC Mtaka

Kwa upande wao Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju na Mwenyekiti wa wakuu wa shule mkoa wa Simiyu, Mwl. Amede Ndonje wamekiri kuwa kambi za kitaaluma zimechangia kuongeza ufaulu katika mitihani ya  kidato cha sita kutoka nafasi ya 26 mwaka 2017 hadi nafasi ya 10 mwaka 2018 na kwa kidato cha nne kutoka nafasi ya 11 mwaka 2017, hadi kufikia nafasi ya tisa mwaka 2018.

  • Maonyesho ya TAFITI UDSM yaanza rasimi
  • Ndugai atoa onyo kali kwa waandishi wa habari Bungeni
  • Wapinzani wasusia bunge, hukumu ya Lema, watoka nje

Katika uzinduzi huo wa kambi za kitaaluma wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Chama na Serikali pamoja na watumishi wa Umma wameahidi kuchangia vyakula ambavyo ni mchele zaidi ya tani mbili, maharage kilo 200, ng’ombe wawili na fedha taslimu ili kufanikisha kambi hiyo kufanyika vizuri.

Wanafunzi wa Kidato cha Sita wako kambini kuanzia tarehe Mosi Aprili, 2019 na wanatarajia kukaa kambini kwa takribani siku 28 na baadaye kutawanyika kwenda kwenye shule zao kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya Mtihani wa Taifa utakaoanza Mei 06, 2019.

JPM amfagilia Mkapa, 'Bila yeye nisingekuwa waziri au Rais'
LIVE: Yanayojiri katika Ziara ya Rais Magufuli mkoani Mtwara

Comments

comments