Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imetakiwa kubadilisha mahali pa kutupa takataka (dampo) kutoka eneo la Ilembo lilipo sasa kwakuwa maji yanayotiririka kutoka katika eneo hilo yanaweza kuelekea katika chanzo cha maji cha Mantengu ambacho kinatarajiwa kuanza kutumika muda si mrefu.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji iliyopo Wilayani humo.

Brig. Jen. (Mst) Mwangela amesema kuwa zoezi la kubadilisha eneo lakutupa takataka lifanyike haraka kwakuwa mradi wa Maji wa Vwawa ambao unatumia chanzo cha Maji cha Mantengu umekamilika na hivi karibuni utaanza kuwafikia wananchi.

“Ile sehemu ya dampo ibadilishwe, maji yameshaanza kutoka na yatawafikia wananchi hivi karibuni, hivyo nawaagiza halmashauri utekelezaji wa hili ufanye haraka,”amesema Brig. Jen. (Mst) Mwangela

Aidha, ameongeza kuwa licha ya kuwa eneo la kutupa takataka litabadilishwa lakini wahakikishe wanazoa takataka zilizopo kwakuwa zikibaki pale zitaendelea kuchafua maji.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo amesema kuwa halmashauri ya Wilaya ya Mbozi itatekeleza agizo hilo na sasa eneo la kutupa takataka litahamishiwa Mbozi Mission ili kulinda chanzo hicho cha maji cha Mantengu.

Jambazi afariki kwa kupigwa risasi na Polisi
Zidane amaliza utata kuhusu tetesi za Pogba kuelekea Real Madrid

Comments

comments