Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amesema kuwa kampeni ya ‘sukuma ndani’ aliyoendesha mkoani humo imesaidia kurudisha watoto wa kike shule kwa asilimia 70 iliyokuwa imetoweka.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na kituo kimoja cha Radio, ambapo amesema kuwa kampeni ile ilikuwa ikihusika na kuwakamata wote watakaohusika na suala la ndoa za utotoni, wakiwemo washenga na viongozi wa dini lakini kwa sasa wameamua kuongeza na jirani wa familia husika.

Amesema kuwa kazi ya jirani ni kusema mabaya anayoyaona kwa jirani yake ili kuokoa katika masuala yasiyofaa, hivyo endapo jirani atakaa kimya atawajibishwa.

“Watu wengi waliona kuwa natania lakini mimi nilikuwa namaanisha na katika ile orodha ya kusukuma ndani wataoshiriki kumuozesha mwanafunzi tumeongeza na jirani, maana huwezi shuhudia jirani yako anavunja sheria ukaacha kutoa ripoti sehemu inayostahili,”amesema RC Mwanri.

Aidha, hivi karibuni alisikika akiwaonya wakurugenzi watendaji wa halmashauri, maofisa elimu mkoani Tabora kutimiza wajibu wao, vinginezo atawaondoa baada ya kupokea taarifa kuwa watoto wa kike zaidi ya 11, 000 hawapo shuleni kwa sababu zisizojulikana.

Ndoa za utotoni nchini bado ni tatizo, huku Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na watoto (Unicef), likitoa ripoti kati ya mwaka 2010 na 2017 inayoonyesha Tanzania inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni baada ya Sudan Kusini na Uganda

Mbaroni kwa kutaka kumpa rushwa polisi
TPDC kuongeza vituo vya kujazia Gesi Asilia