Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amewaagiza wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kuchapa kazi kwa kuzingatia uweledi, ili kuepuka vitendo vya Rushwa.

Senyamule, ameyasema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi wa LATRA iliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo jijini Dodoma na kuwaagiza kuchukua hatua dhidi ya madereva na wasafirishaji wanaokiuka Sheria za matumizi sahihi ya miundombinu ya usafirishaji, na kusababisha ajali.

Amesema, serikali imewekeza fedha nyingi katika maendeleo ya miundombinu ya barabara na reli nchini, kuna baadhi ya madereva na wasafirishaji wanashindwa kutimiza wajibu wao na kusababisha maafa na taharuki kwa watumiaji wengine wa miundombinu hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.

“Sisi Dodoma tumebahatika kupata miundombinu mizuri ya usafiri wa barabara na reli, LATRA muendelee kutoa elimu ya matumizi sahihi ya miundombinu kwa umakini na kwa kufuata taratibu sahihi ili kukamilisha azma ya Serikali ya kuwezesha maisha bora kwa Watanzania” Alisisitiza.

Aidha, amesema mazingira ya wafanyakazi wa LATRA yanavishawishi vingi kutokana na mgongano wa maslahi ya watoa huduma mbalimbali hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa uweledi na uadilifu ili kuboresha huduma inayotolewa kwa wananchi na kuepusha migogoro.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa LATRA, Habibu Suluo amesema Mamlaka hiyo imepewa jukumu la kudhibiti usafiri wa Reli ,usafiri kwa njia ya barabara ,na usafiri wa waya huku akisema kwa upande wa reli wanadhibiti reli ya kati na reli ya Tazara.

Makalla: Hongereni kwa CEO mzuri
NECTA: Hakuna shule wala mwanafunzi bora