Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Elias Mwangela amewataka Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) kukamilisha miradi ya ujenzi wanayopewa ndani ya muda wa makubaliano ya mikataba.

Ameyasema hayo wakati akishuhudia utiaji saini wa mikataba miwili ya ujenzi wa Nyumba ya Mkuu wa Mkoa na ya Katibu Tawala Mkoa kati ya TBA na Katibu Tawala Mkoa wa Songwe.

Amesema kuwa TBA wamechelewesha ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na ujenzi wa Hospitali ya Mji wa Tunduma hivyo ucheleweshaji huo usirudie tena katika mikataba hiyo miwili waliyopewa kwani hatasita kuvunja mikataba hiyo endapo wataonyesha ucheleweshaji.

“TBA mna sifa nzuri ya kujenga majengo ya serikali kwa kuzingatia ubora unaotakiwa na kwa gharama nafuu lakini kuna wakati kunakuwa na kusita katika kuwapa kazi kutokana na historia yenu ya kuchelewesha kukamilisha miradi mnayopewa ya ujenzi,” amesema Brig. Jen.  Mwangela.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, David Z. Kafulila ameishukuru serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuupatia Mkoa wa Songwe kiasi cha shilingi bilioni 26.8 kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali mkoani humo.

Aidha, amesema kuwa serikali imekuwa ikitoa fedha za miradi mbalimbali lakini kasi ya utoaji wa fedha na matumizi ya fedha hizo kwenye miradi husika imekuwa haiendani na hivyo kusababisha kuchelewa kukamilika kwa miradi hiyo.

Hata hivyo, kwa upande wake Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Songwe Mhandisi, Fidelis Cosmas ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwaamini na kuwapa miradi hiyo miwili yenye thamani ya shilingi bilioni moja na kuahidi kuikamilisha kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

 

Simba yaongeza nguvu Ligi ya Mabingwa Barani Afrika
Ole Sendeka atoa maagizo,' Sasa kuanza na wenyeviti'