Wababe wa mjini Madrid nchini Hispania (Real Madrid) wameingia katika majaribu mazito, kufuatia kuuamia kwa nahodha na beki wao Sergio Ramos akiwa katika majukumu ya timu ya taifa usiku wa kuamkia hii leo.

Ramos alilazimika kutolewa uwanjani katika dakika ya 80, kufuatia maumivu ya goti ambayo yalionyesha kumtesa, licha ya kupatiwa huduma ya kwanza.

Kocha mkuu wa taifa ya Hispania Julen Lopetegui, alithibitisha katika mkutano na waandishi wa habari kwa kusema Ramos anasumbuliwa na maumivu ya goti na hii leo atafanyiwa vipimo mara baada ya kurejea mjini Madrid wakitokea Albania, ambapo walikwenda kucheza mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia na kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri.

Kuumia kwa beki huyo mkongwe katika kikosi cha Real Madrid, kunaendelea kuleta hofu kwa meneja Zinedine Zidane, ambaye ataendelea kuwakosa Marcelo, Casemiro pamoja na Luka Modric.

Taarifa za awali zinadai kuwa, Ramos huenda akawa nje ya uwanja kwa majuma matatu mpaka manne na anatarajiwa kukosa michezo ya ligi ya Hispania dhidi ya Real Betis, Athletic Bilbao, Alaves pamoja na Leganes (Ligi Ya Mabingwa Barani Ulaya).

Pia anatarajiwa kuukosa mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 dhidi ya Macedonia utakaochezwa Novemba 12 pamoja na mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Uingereza utakaochezwa Novemba 15.

Video: Baraka The Prince akerwa na utani wa Stan Bakora, "iwe mwanzo na mwisho"
Gerard Pique Kutoa Nafasi Kwa Vijana