Rais wa klabu ya Sevilla CF Jose Castro ameonyesha kukata tamaa katika harakati za kumsajili mshambuliaji kutoka Jamuhuri ya Dominica na klabu ya Olympique Lyonnais ya Ufaransa, Mariano Díaz Mejía.

Sevilla CF ilionyesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo mzaliwa na Hispania, lakini kuingia kwa klabu ya Real Madrid kumewaogopesha na kutangaza kusalimu amri.

Castro amesema hawawezi kuendelea na mchakato wa kumsajili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25, kutokana na ushindani uliopo dhidi ya Real Madrid, ambao wanawahofiwa huenda wakaongeza thamani ya usajili wa mchezaji huyo.

“Tulijaribu kumsajili, lakini kwa sasa tunasema tunajiondoa rasmi katika mchakato huo na kuwaachia wengine ambao wana uwezo wa kumsajili kwa kiasi chochote cha pesa,” Alisema Castro.

“Madrid wana nguvu kubwa katika ushawishi wa kumsajili mchezaji yoyote duniani, na ukizingatia Mariano aliwahi kuwa mchezaji wao tangu akicheza katika ngazi ya soka la vijana, hivyo itakua rahisi kwao kumpata.”

“Lakini mpaka sisi tunafikia maamuzi haya, mchezaji mwenyewe hajawahi kusema lolote kuhusu muelekeo autakao, lakini tumeona hakuna haja ya kupambana na wenye pesa na kufikia hatua ya kumpandisha thamani mchezaji.”

Kwa maamuzi hayo Real Madrid watakua na kila sababu ya kufanikisha usajili wa Mariano kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi ndani ya saa 24 zijazo.

Mariano aliwahi kupita katika kituo cha kukuza na kulea vijana cha Real Madrid kuanzia mwaka 2011-2012, akisajiliwa kutoka Badalona ya Cataluña.

Kati ya mwaka 2012 hadi 2014 alicheza katika kikosi cha  Real Madrid C na kufunga mabao 18 katika michezo 46, mwaka 2014–2016    alipandishwa na kucheza katika kikosi cha Real Madrid B, ambapo alifunga mabao 32 katika michezo 44, na mwaka 2016–2017 alicheza kwenye kikosi cha wakubwa cha Real Madrid alifunga bao moja katika michezo 8.

Aliuzwa Olympique Lyonnais ya Ufaransa kwa Euro milioni 8 na mpaka sasa ameshaitumikia klabu hiyo katika michezo 37 na kufunga mabao 18.

Benki ya Standard Chartered kuipatia mkopo Tanzania
Yaya Toure afanya vipimo London, kusajiliwa kimya kimya