Mwanasheria, Mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake na watoto na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Msichana Initiative, Rebeca Gyumi, pamoja na wenzake watatu wameshinda tuzo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka huu wa 2018.

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa, kupitia ukurasa wake wa Twitter amewapongeza kwa mchango wao wa kusongesha mbele haki za binadamu.

Kwa mujibu wa BBC, Rebeca na washindi wengine watatu wa mwaka huu watapatiwa tuzo yao mjini New York, Marekani tarehe 10 Desemba mwaka huu, wakati wa kilele cha tamko la haki za binadamu la umoja wa mataifa ambalo mwaka huu linatimiza miaka 70.

  • Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Msichana Initiative

Mshindi mwingine ni Asma Jahangir mwanaharakati na mwanasheria wa Pakistani ambaye amefariki dunia mwaka huu.

“Kile tumekuwa tukikifanya ni kuwahamasisha wasichana kusimamia ndoto zao na kuzifikia katika jamii, kitu ambacho kimechukuliwa kuwa cha umuhimu,” “Kwetu ni furaha kuwa dunia imetambua kile tukifanya na sasa ni fursa muhimu kuzungumzia changamoto ambazo wasichana wanapitia, na kuihamasisha serikali na wadau kuweza kuona faida ya mtoto wa kike katika maendeleo ya jamii,” Bi Gyumi aliiambia BBC.

Mwanasheria huyu alishinda kesi kubwa mwaka 2016 iliyohusu ndoa za watoto baada ya kupinga sheria ya ndoa ya mwaka 1971 nchini Tanzania, iliyoruhusu wasichana wenye miaka 14 kuolewa.

Kutokana na kazi yake ya kupigania haki ya msichana, Bi Gyumi ameshinda tuzo ya UNICEF ya mwaka 2016 na kutajwa kuwa mwanamke wa mwaka na jarida la New African Women.

 

Mama apoteza watoto 3 kwa kujiua wenyewe
Waziri aomba radhi kuvuja kwa picha zake za ngono