Imefahamika kuwa Wapinzani wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya Mtoano Red Arrows ya Zambia, watawasili Jijini Dar es salaam leo Ijumaa (Novemba 26), tayari kwa mchezo wa mkondo wa Kwanza.

Simba SC itakuwa mwenyeji wa mchezo huo, Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam siku ya Jumapili (Novemba 28), kisha itakwenda ugenini nchini Zambia kucheza mchezo wa Mkondo wa pili Desemba 05.

Uongozi wa Red Arrows umeweka wazi kuwa Msafara wao unatarajia kuwasili nchini leo ijumaa (Novemba 26) usiku tayari kwa mchezo wao dhidi ya Simba SC.

Meneja wa timu hiyo, Rio Flowers amesema: “Tupo kwenye maandalizi ya mwisho ya kujiandaa kuja huko kwa ajili ya mchezo wetu.”

“Safari yetu ya kuja huko tunategemea itakuwa siku ya Ijumaa ingawa bado sijajua itakuwa ni saa ngapi lakini kuna uwezekano wa kuingia huko usiku, jambo kubwa ni kwa wachezaji wetu kuweza kuendana na hali ya hewa ya huko japo kuwa haitofautiani na ile hapa kwetu.”

Jana Alhamis (Novemba 25) Msaidizi wa Afisa Habari wa Simba SC Ally Sharty alizungumza na Dar24 Media na kueleza kuwa, wapinzani wao walikua kimya kuhusu ujio wao hapa nchini, jambo ambalo liliwafanya kufuatilia kwa ukaribu ili kujua ni lini watawasili.

Simba SC iliangukia kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kutolewa kwenye Michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa kufungwa nyumbani Dar es salaam mabao 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Kabla ya mchezo huo Simba SC ilishinda ugenini mjini Gaborone mabao 2-0, hivyo Mabingwa hao wa Tanzania Bara walitupwa nje kwa kufungwa mabao mengi nyumbani.

Kocha Red Arrows aitambia Simba SC
Bangala kuikosa Mbeya kwanza FC