Klabu ya Red Arrows ya Zambia mpaka sasa haijatoa taarifa za safari ya kuelekea Jijini Dar es salaam, kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika Hatua ya Mtoano.

Red Arrows itacheza dhidi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC siku ya Jumapili (Novemba 28), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Akizungumza na Dar24 Media, Msaidizi wa Afisa Habari wa Simba SC Ally Sharty amesema mpaka sasa hakuna taarifa zozote za ujio wa wapinzani wao.

Amesema Uongozi wa Simba SC unaendelea kufuatilia ni lini na muda gani Msafara wa Red Arrows utawasili Jijini Dar es salaam.

“Hatujapata taarifa zozote mpaka sasa kuhusu ujio wa hawa jamaa, tunaendelea kufuatilia ili kufahamu lini na muda gani watawasili,” amesema Sharty

Katika hatua nyingine Ally Sharty amewataka Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumapili (Novemba 28), ili kuipa nguvu timu yao ambayo inahitaji ushindi utakaoiweka kwenye mazingira mazuri kabla ya mchezo wa mkondo wa pili utakaochezwa nchini Zambia Desemba 05.

“Mashabiki wanapaswa kuitikia wito wa kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa, wanatakiwa kuipa hamasa timu yao ili kufikia lengo la kushinda mchezo huu ambao tuko nyumbani.” amesema Sharty.

Simba SC iliangukia kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa Ligi Mabingwa Barani Afrika kwa kufungwa na Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Chriss Mugalu atabiriwa Makubwa Msimbazi
Mashabiki 35,000 waruhusiwa Kwa Mkapa