Na Matilda Spicegirl

“Upendo na huruma ni vitu vya umuhimu katika uhusiano ni kama mzizi katika ua, hivyo ukikatwa hakuna kustawi tena,” naanza kwa kumnukuu Dalai Lama, mtaalam wa masuala ya uhusiano.

Mahusiano ya aina yoyote ile siyo kitu rahisi, iwe kati yako na mpenzi wako, kaka, dada, mama, baba au hata rafiki yako. Kibinadamu hakuna mtu aliye mkamilifu.

Unaweza kuwa kwenye mahusiano hususan ya kimapenzi ukiwa na mategemeo makubwa juu ya mwenzako. Lakini ukajikuta katikati ya changamoto kama kushindwa kuomba unachohitaji kwakuogopa matokeo yake, kupenda ushindani, kuwa mtu wa kujishtukia au kumshtukia mwenzi wako, waweza kuwa tegemezi kwa mwenzi wako  na mambo mengine mengi.

Lakini dawa chanya ya changamoto ya aina yoyote katika mahusiao ya aina yoyote ile yenye lengo jema ni kujitambua na kujiweka katika hali sahihi kuliko kutafuta ukamilifu wenye lengo la kumfurahisha mwingine.

Mahusiano ni magumu pia kwani yanakuwa kama kioo  cha jinsi ambavyo mtu unajisikia kwa wakati fulani.

Wataalam wa saikolojia wanasema kuwa uhusiano ni kama kioo, mtu anavyojiweka na kuamini ndivyo alivyo katika jamii, ndivyo atakavyoiona taswira yake kwenye jamii hiyo.

Uhusiano Usio na Furaha

Hii ina maana kwamba kama uko katika uhusiano wa mapenzi au urafiki wa karibu sana, wakati ambapo utahisi una furaha sana moyoni mwako hata kama ni ya kuitengeneza, ndivyo utakavyoona uhusiano wenu ni wa furaha. Lakini ukianza kutengeneza ghasia moyoni mwako siku hiyo, utaona uhusiano wako pia uko katika hali ya ghasia.

Mfano ukiwa na siku mbaya utaona kila anayekuzunguka ni ghasia  au ukiwa una furaha moyoni utakuwa unaona kama mahusiano yako na mwenzi wako yana mapungufu kumbe hili hutokea pale tu unaposhindwa kujitambua na kufahamu kuwa hisia zako na uamuzi wako vina nafasi kubwa katika kufanya marekebisho kabla hujamgusa mwenzi wako. Anza na wewe kwanza. Usiwe mwepesi kutupa mpira wa lawama kwa mwenzio ukitafuta utetezi ili uonekane wewe mwema zaidi na unaonewa.

Kama umewahi kuwa katika mikwaruzo na rafiki, mpenzi au ndugu na kujikuta mwishoni ukijihoji ni nini hasa kilichokukwaza, au umewahi kukatishwa tamaa kwa sababu mtu fulani au mpenzi wako hakukidhi matarajio yako hivyo ukajisikia kama mtu asiyesikilizwa , makala hii inaweza kuwa msaada kwako kwa njia moja au nyingine.

Yafuatayo ni mambo yanayoweza kukusaidia kujibu maswali uliyonayo au kutoa ufumbuzi wa tatizo fulani ulilonalo katika mahusiano;

  1. Fanya kitu moyo wako unapenda

Kila mtu huwa na mahitaji na machaguo yake katika maisha ya kila siku. Mfano, kuna wengine hupenda kulala sana wanapopata muda, kwenda matembezini, kuangalia ‘filamu’na kadhalika.

Unapkuwa na mtu ambaye una uhusiano naye kama rafiki au mpenzi akataka muanze kuishi tofauti na ulivyokuwa umezoea, hata kama una shauku kiasi gani na uhusiano huo, usikurupuke na kufuata njia zake. Tafakari kwa kina, jaribu kufikiri faida na hasara kisha fanya maamuzi yasiyouumiza moyo wako. Fanya kile moyo wako unapenda. Lakini hii haimaanishi kuwa hauwezi kufanya ‘sacrifice’ , lakini fikiria na jiridhishe ili moyo wako upende unachotaka kufanya huku ukimridhisha mwenzako.

2. Epuka hisia mbaya dhidi ya mwenzio

Ni kweli kuwa hupaswi kumuamini mtu yoyote kwa asilimia zote, lakini isiwe chanzo cha kujenga hisia mbaya kwa mtu uliye na uhusiano naye mara kwa mara. Kama unahisi kuna sehemu hayuko sawa, ni vyema ukafuatilia na kumsaidia. Mkanye na mueleze ukweli ukiwa na uhakika na unachokifanya.

Hisia mbaya zinaweza kusababisha rafiki, mpenzi au hata ndugu yako akaanza kukuogopa kwa kuwa anajua humuamini na sivyo alivyodhani mnaendana. Mwisho wa siku anaweza kuwaza kukufanyia hata kile ambacho hakuwa na wazo nacho.

Katika mahusiano mtu yoyote anayekujali hatopenda kukuumiza bila sababu, bali angependa kukuona siku zote ukiwa mwenye furaha. kwahiyo huenda kashindwa fanya jambo fulani la kukufurasha kama kwenda ‘out’,  sababu ya kutingwa sana na kazi au sababu nyingine. Badala ya kufikiria vibaya, mshirikishe kwa ukaribu kile unachofikiria kwa mtazamo chanya.

3. Jitazame kwanza kugundua tatizo

Ukiwa huna furaha katika mahusiano ni rahisi sana kuhisi kuna tatizo kwenye mahusiano yenu. Kama utakuwa ni mtu wa kutupa lawama kwa mwenzio basi tambua utatuzi wa tatizo hilo utakuwa kwa mlengwa kwani kwa kufanya hivyo kunamfanya kwanza kuwa na ‘control’, pili kutoleta utatuzi  wa tatizo lako mara nyingi kwani wewe mwenyewe haujatafuta mzizi wa tatizo.

Iwapo utajisikia uhitaji wa kumlaumu mwingine kwa hisia zako, kitu alichokufanyia au ulichotakiwa kufanya, kwanza kabisa jiulize je kuna kitu kingine zaidi ya hicho kinachokusibu?

Kwa sababu mara nyingi unaweza kukuta kuna kitu tofauti kinakuandama ndani yako bila kugundua mapema. Iwe ulichofanya au ulichotakiwa kufanya na hukufanya. Hicho kinaweza kuwa chanzo kinachokukosesha raha na sasa unatafuta sababu nje yako na kuishia kumlaumu asiyehusika.

4. Tambua, Kubali mapungufu yako

Kwa jinsi binadamu wengi, binadamu wengi tulivyo ni vigumu sana kuukubali udhaifu wetu. Hivyo, mara nyingi hujikuta tukijaribu kujibambikia tabia isiyo yatu. Mfano wewe unaweza usiwe rafiki mwaminifu, lakini unaweza kujikuta unaupeleka udhaifu huo kwa rafiki yako na kumlaumu yeye huku ukijiona wewe sio chanzo cha tatizo. Inakuwa kama tabia fulani hivi uliyojijengea ya kujilinda ili kukwepa kukiri mapungufu uliyonayo.

Kwahiyo, jaribu siku zote kujichunguza mapungufu yako kabla hujaanza kumyooshea kidole mwingine. Hii itakusaidia kujifunza zaidi jinsi ya kubadilika na kuwa mtu bora zaidi ya ulivyo.

5. Chagua uzito wa tatizo lako

Kuna baadhi ya watu ambao ugomvi ni sehemu ya maisha yao, karibu kila wanachofanya huishia kugombana. Unapotofautiana nao mawazo tu, kwao hugeuka kuwa ugomvi badala ya kuwa mjadala. Unaweza kuwa na rafiki ambaye hata kumsifia tu huleta mabishano!

Ili kuleta amani ni vyema ukapima umuhimu wa kitu unachotaka kutolewa majibu au ufafanuzi. Kama siyo kitu cha muhimu sana unaweza kukipotezea kabisa ili kuepuka mifarakano.

6. Mkabili mwenzio kwa upole na uwazi

Binadamu tumeumbiwa hofu inayopelekea kujilinda kwa mambo mengi (defensive). Ukimshambulia mwingine, kibinadamu na yeye atajaribu kujitetea hali ambayo haitawapeleka popote au kutatua chochote. Mara nyingi mtaishia kumtafuta mshindi na kila mmoja akitaka kujilinda ili wazo lake lionekane bora zaidi.

Lakini ni vyema kuwasilisha wazo lako na kutoa nafasi ya mjadala ukiufungua moyo wako kukubali wazo bora zaidi la rafiki, mpenzi, ndugu au jamaa yako. Mfano mzuri hapa, ni wakati wa siasa, mpira na mambo mengine. Uhusiano huwa hatarini pale wawili wanapotofautiana mawazo na wakashindwa kutumia busara zaidi.

Unapaswa kufahamu kuwa kutofautiana mtazamo na mawazo ni chachu ya maendeleo ya kila kitu kwani mwisho wazo bora zaidi hupatikana. Lakini ikiwa vinginevyo, tofauti hii inaweza kuzua balaa badala ya baraka.

7. Usiogope kujishusha

Katika mahusiano kuna namna mbalimbali ambapo unaweza kujishusha ili kumpa nafasi mwenzako. Usiwe mfalme au malkia wakati wote, atajiona mtumwa wako. Mfano, pale unapomfahamisha mwenzi wako kuhusu hisia zako juu yake, au pale unapokuwa muwazi kuhusu nafsi yako au maisha yako ya nyuma, pale unapokiri kosa na kadhalika. Unakuwa umejishusha kwa sababu nzuri. Usifanye tu mambo ilimradi kuonekana una nguvu katika mahusiano.

8. Tafakari kabla ya kutenda jambo

Fikiria

Hii ni moja ya vitu muhimu sana na kwa kutamka unaweza kudhani kila mmoja anafanya, lakini ni vigumu sana watu wenye hisia fulani kutekeleza hili. Inahitaji nguvu ya ziada ya akili na kujenga utamaduni.  Wengi baada ya kuumizwa, kuwa na hasira au kuvunjwa moyo hutamani kufanya lolote ili kupata ahueni wakati huo huo kitu ambacho ni vibaya. Unaweza kuamua kufanya jambo fulani kwa hasira lakini baada ya kukaa dakika chache, utagundua kuwa ni kosa kubwa ulilowahi kulifanya maishani na huenda ikakugharimu.

Usitume ujumbe ukiwa umekasirika, usipige simu kuongea na rafiki, mpenzi au ndugu ambaye amekuudhi sana. Unaweza kujikuta unavunja kabisa uhusiano wenu kwa kitu ambacho mgeweza kukaa chini mkaeleweshana.

9. Jifunze kutambua na kuheshimu mipaka

Watu wengi wakiwa na ukaribu sana ni vigumu kuvuka mipaka au kutoiona kabisa. Katika mahusiano yasiyo na mipaka ni rahisi sana kumruhusu mwingine kukuhadaa ili kufanya vitu ambavyo wewe mwenyewe hutaki au hupendezewi navyo na kuamua kufanya tuu ili kumridhisha au kufanya tu ‘out of guilt’ badala ya kuridhisha roho yako.

Pima uhusiano wenu, tambua umefikia hatua gani. Hesabu maneno yako na tofautisha nyakati ili usivuke mipaka na kujikuta unamkwaza au ana kukwaza bila kutarajia. Unapoanzisha utani, fikiria kama mmefikia hatua hiyo na mnataniana kwa kiwango kipi? Usipoweza kuiona mipaka utazua vita.

10. Furahia uwepo wa mwenzio zaidi ya kukubalika kwako

Katika uhusiano, ukiwa ni mtu wa kutafuta kukubalika kila mara basi ujue mahusiano yenu kwako yatakuwa yanahusu nini mwenzi wako anachokufanyia. Ni kwa kiasi gani anakufurahisha ukiwa kwenye huzuni, anakuridhisha kwa kiasi gani, na mengine mengi.

Tabia hii inaweza kumchosha mwenzi wako na anaweza kujihisi kama amekuwa mtumwa kwako. Unapaswa kufikiria pia wewe unamfanyia nini?

Jitahidi sana kufurahia uwepo wenu mkiwa pamoja. Hakuna kitu kizuri kama kupuuzia vitu vidogo na kujipa mwenyewe nafasi ya kufurahia mahusiano yenu. Usiwe wa kulalamika tu na kutegemea makuu wakati wewe mwenyewe hata haujigusi kuhakikisha hayo yanafanyika kiurahisi. Usifanye mambo hayo kuwa kama deni kwa mwenzio.

Epuka kuwa mtu wa kulaamika muda wote, kuwa mtu wa shukurani na mwepesi wa kumfanyie mwenzi tendo jema kama ambavyo ungependa kufanyiwa.

Hali hii itadumisha uhusiano wenu wa aina yoyote wenye tendo jema, na kuwafanya kuwa watu mnaotegemeana badala ya wewe kuwa mtegemezi.

 

 

Azam FC Wadhamiria Kulipiza Kisasi
Falcao Kutimka Chelsea