Mwanafamilia wa lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Rich Mavoko ameridhia ‘kutupia’ fulana ya mkali wa ‘Seduce Me’, Ali Kiba.

Mavoko ambaye kabla ya kujiunga na WCB akiwa kama msanii anayejitegemea alitajwa kuwa mmoja kati ya wasanii wenye ushindani mkubwa akimfuatia Bosi wake wa sasa, Diamond Platinumz, amesema haoni tatizo kuvaa fulana iliyoandikwa ‘King Kiba’ na kupiga picha.

Kauli hiyo ya Mavoko anayefahamika pia kama Messi imekuja kufuatia swali aliloulizwa na mtangazaji wa Times FM, Jonijoo kupitia kipindi chake maalum kwenye YouTube kinachoitwa ‘Now You Know’.

“Nina zawadi yako, nina T-shirt hapa imeandikwa ‘King Kiba’ nataka uvae halafu tupige picha,” linasikika swali la Jonijoo.

“That’s easy (hiyo rahisi), naweza… tunaweza kupiga na picha. Kwanini tusipige picha?” Rich Mavoko alijibu na kuhoji kwa wakati mmoja.

Hivi karibuni, kuliibuka ushindani mkali ulioibua hisia tofauti kwa mashabiki baada ya WCB kuachia video ya wimbo wake ‘Zilipendwa’, muda mfupi baada ya Ali Kiba kuachia ‘Seduce Me’.

Hata hivyo, taharuki kati ya wasanii hao iliibuka zaidi kufuatia majibishano ya msigano kati ya Ali Kiba na Diamond baada ya Bosi huyo wa WCB ‘kumchana’ Ali kwenye remix ya wimbo ‘Fresh’ wa Fid Q. Ali naye alijibu kupitia Twitter, mgogoro ambao baadae ni kama ulizimwa na majibu yenye ‘ukakasi’ kutoka kwa Ommy Dimpoz.

Katika hatua nyingine, Mavoko ambaye wimbo wake ‘Sheri’ aliomshirikisha Fid Q unafanya vizuri, alisema kuwa kabla ya kuachia wimbo asubuhi, hufanya dua (maombi) usiku ili upokelewe vizuri.

Aidha, alisema kabla ya kupanda kwenye jukwaa lolote huangalia kwanza matamasha yanayofanywa na wasanii wakubwa wa nje ya nchi.

Mavoko ni mmoja kati ya wasanii waliofunika katika jukwaa la Fiesta mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Arusha.

Video: ADC walaani kushambuliwa kwa Lissu
LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Septemba 11, 2017