Mbunge wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ridhiwan Kikwete amewataka wenyeviti wa serikali za mitaa pamoja na madiwani wa chama hicho kufanyakazi kwa ushirikiano ili kuweza kutatua kero mbalimbali za wananchi.

Ameyasema hayo jimboni humo wakati wa kikao cha halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Pwani, ambapo amewataka kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuweza kusimamia vizuri miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amewataka wajumbe hao kuwa wamoja na kufanyakazi kwa ushirikiano wa karibu na wananchi ili kuweza kutambua kero mbalimbali zinazowakabiri katika maeneo husika wanayo yaongoza na kuzitatua.

”Ndugu zangu nawaomba tufanyekazi kwa ushirikiano, ushirikiano ndio kila kitu katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM, kama ukimuona jirani yako anamatatizo msaidie, sisi wote ni wamoja,”amesema Kikwete

Akizungumzia kuhusu suala la kuimarisha chama, amewataka wajumbe hao kushikamana katika kusimamia miradi ya maendeleo ili kuweza kufikisha huduma stahiki kwa jamii iliyowaamini na kuwakabidhi dhamana ya uongozi.

Aidha, wajumbe hao ambao walikuwa wamekutana kwaajili ya kuzungumzia kero mbalimbali zinazowakabiri katika maeneo yao wanayoyaongoza, wamemuomba mbunge huyo kuwa nao karibu ili kusaidia katika masuala mbalimbali hasa katika kusimamia miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainab Kawawa amewataka wajumbe hao kusaidia kutatua migogoro mbalimbali ukiwemo mgogoro wa wakulima na wafugaji. ambao umekuwa ukigharimu maisha ya watu.

Nao wajumbe hao wakiwemo wenyeviti na madiwani wamemuomba mbunge huyo wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete kuingilia kati baadhi ya migogoro ya miradi ya maendeleo ambayo imekuwa ikikwamishwa na baadhi ya watendaji.

Mwigulu amjibu Zitto Kabwe 'Usivyo na utu huoni utu unaona siasa'
Kituo cha watoto chafungwa kwa tuhuma za kunajisi wavulana