Uongozi wa klabu ya Young Africans umetakiwa kuweka mambo hadharani kuhusu mustakabali wa kocha mkuu Hans Van der Pluijm ambaye inasemakana huenda akaondolewa katika nafasi hiyo.

Ombi hilo limetolewa na mwanachama Young Africans Ridhiwani Kikwete alipozungumza na Times FM mapema hii leo katika kipindi cha Sunrise.

Ridhiwani amesema ipo haja kwa viongozi wa klabu hiyo kumaliza utata uliojengeka baina ya uongozi, wanachama pamoja na mashabiki, ambao wanataka kufahamu mustakabali wa kocha huyo kutoka nchini Uholanzi.

Amesema tayari inafahamika uongozi wa Young Africans upo mbioni kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi kwa kutaka kumpa nafasi aliyekua kocha mkuu wa Zesco United ya nchini Zambia George Lwandamina, ambaye ameripotiwa kuwa nchini tangu juma lililopita.

“Imefikia wakati viongozi wa Young Africans wazungumze ukweli wa suala hili, ili mambo mengine yaendelee klabuni, minong’ono imekua mingi kuhusu mabadiliko ya benchi la ufundi, japo kila mmoja amekua anasema la kwake kuhusu ujio wa kocha mpya.”

“Itapendeza kuona kila jambo linafanyika na kumalizwa kwa wakati ili shughuli nyingine ziendelee hasa suala la usajili ambalo kwa sasa linaendelea kufanyika katika klabu zote za ligi kuu.” Alisema Ridhiwani.

Hata hivyo Ridhiwani Kikwete ambaye aliwahi kuwa makamu mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Young Africans, amekiri kufahamu uwezekano George Lwandamina kukabidhiwa jukumu la kuwa kocha mkuu badala ya Hans Van der Pluijm.

“Mimi ninafahamu kwamba Lwandamnina ndio kocha mpya wa Young Africans japo suala hili linafichwa, na ninashangaa kwa nini linaendelea kuweka kapuni hadi sasa.”

“Viongozi wanatakiwa kuwa na kauli ya mwisho, kama ilivyo katika nyumba zetu, ambapo baba ama mama akisema jambo fulani, ndilo linatakiwa kuheshimiwa na kuaminiwa” Aliongeza Ridhiwani.

Wakati huo huo Ridhiwani amekiri kupendezwa zaidi na uwezo wa kocha Hans Van der Pluijm tangu alipotua klabuni hapo mwaka 2013, ambapo ameiongoza Young Africans kutwaa ubingwa wa Tanzania bara mara tatu, kombe la shirikisho mara moja na kuifikisha klabu hiyo katika hatua ya mtoano ya michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika.

“Huyu kocha ni bora kwangu na ninaamini hata kwa wanayanga wengine ni bora pia, kwa sababu tangu alipofika hapa nchini kumekua na mabadiliko makubwa katika kikosi chetu, tumefanikiwa sana, hivyo kuondoka kwake huenda ikawa changamoto ya mafanikio zaidi ama jambo lingine”

“Hata kwa msimu huu amejitahidi sana, ukiangalia kulikua na pengo kubwa kati yetu na Simba ambao walionyesha soka safi mwanzoni mwa msimu, lakini alijitahidi kupunguza pengo kutoka pointi nane hadi sasa tunapitwa kwa pointi mbili na watani zetu wa jadi.” Alisema.

Bashe: Mfumo wa kupata viongozi ndani ya CCM ni gulio
Yaya Toure Kusajiliwa Ligi Ya Mabingwa Barani Ulaya