Makali ya Mahakama ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi ambayo majengo yake yako mbioni kuanza kuandaliwa katika maeneo ya Sinza jijini Dar es Salaam, yanadaiwa kuanza na sakata la Richmond.

Sakata hilo la Richmond lilisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa kujiuzulu nafasi yake hiyo mwaka 2008 baada ya ripoti ya Kamati Maalum ya Bunge iliyokuwa chini ya Dk. Harrison Mwakyembe kuwasilishwa Bungeni. Ripoti hiyo ilibaini kuwa kampuni ya Richmond Development Company LLC iliyopewa zabuni ya kufua umeme ilikuwa kampuni hewa.

Gazeti la Raia Mwema limeeleza kuwa chanzo chake cha kuaminika kimebainisha kuwa Rais John Magufuli tayari ameshasaini muswada wa sheria ya uhujumu uchumi hivyo imeshakuwa sheria kamili inayotarajiwa kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali muda wowote. Chanzo hicho kimelieleza gazeti hilo kuwa vigogo watatu wa Serikali ya Awamu ya Nne watakuwa wa kwanza kufikishwa katika mahakama hiyo kutokana na sakata la Richmond.

“Zaidi ya Lowassa, Waziri Mwingine wa Serikali ya JK aliyejiuzulu wadhifa wake kutokana na kashfa hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Uhusiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi,” Raia Mwema imeandika. Bila shaka hawa ndio vigogo watatu wanaotajwa hapo juu.

Lowassa ambaye mwaka jana aligombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa amekuwa akikanusha kuhusika na Richmond akidai kuwa ameonewa na kwakuwa Kamati ya Mwakyembe ilichukua uamuzi bila kumhoji. Amekuwa akisisitiza kuwa mwenye ushahidi kuhusu tuhuma hizo ampeleke mahakamani.

Majaji 14 wamechaguliwa kuamua kesi katika mahakama hiyo na wanatarajiwa kuanza mafunzo katika Chuo Cha Sheria kilichoko Lushoto, Tanga.

Audio: Kufuatia picha zinazosambaa kuhusu ajali ya Ngorika na Ratco Polisi Pwani wamezungumza haya
Oscar Pistorius atupwa jela Miaka 6 kwa kumuua mpenzi wake