Utafiti uliofanywa na gazeti la PM Express la nchini Nigeria umebaini kuwepo idadi kubwa ya wanawake wanaolalamika kukosa wanaume wenye sifa za kuanzisha nao familia, kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, wanawake wengi wameeleza kuwa wamekosa wanaume wa kuolewa nao kwa sababu ya kukosa matumaini ya siku za usoni za wanaume wanaowachumbia kuwa na sifa za kuwa baba bora wa familia, na kukosa wanaume walio na utayari kuoa.

Ripoti imebaini kuwa wanawake wengi wanaona bora kuishi peke yao au kuishi nyumbani kwao kuliko kuishi na mwanaume ambaye maisha yake ya usoni hayaoneshi mwanga wa kumudu maisha.

Lakini pia, wanaume wenye umri mkubwa waliohojiwa ambao hawajaoa, wengi wao walieleza kuwa ni bora waishi peke yao kuliko kuingia katika maisha ya ndoa ili hali hawana uhakika wa vipato vya kumudu maisha ya kisasa ya wanawake.

Hata hivyo, kwa mujibu wa utafiti huo, wanawake wengi wenye umri mkubwa wameonesha kulalamika kukosa wanaume ingawa wanatamani kuolewa, huku wakidai kuwa muda wao kiafya wa kuzaa watoto (ukomo kati ya miaka 45-50) unawapa wakati mgumu.

Karia Anumba, mwenye umri wa miaka 41, mmoja kati ya wanawake waliohojiwa na PM.PRESS ameeleza kuwa amezunguka majiji kadhaa nchini humo akijaribu kumpata mwenzi wake bila mafanikio. Ameeleza kuwa wachumba wengi aliofanikiwa kuwa nao katika baadhi ya majiji walionesha kuogopa kuoa kwa madai ya kutokuwa na uhakika wa maisha ya ndoa.

Ameeleza kuwa akiwa Abuja, aliwapata wanaume kadhaa aliokuwa na uhusiano nao, lakini licha ya kuwashawishi kuwa angeweza kuhudumia familia yeye mwenyewe kutokana na kipato chake, hakuna aliyekubaliana naye kufikia hatua ya kufunga ndoa.

Anumba ameeeleza kuwa alihamia Lagos kikazi akitokea Abuja, lakini kutokana na msako wake wa mwanaume wa maisha yake alifikia hatua akajiona kuwa anageuka kuwa kahaba kutokana na ongezeko la idadi ya wachumba.

Gazeti hilo limemkariri pia Doris, ambaye ana umri wa miaka 39 (jina la baba yake limehifadhiwa), ambaye alidai kuwa amewahi kuwa na wachumba wengi na kuwaonesha maisha ya mapenzi yaliyo na raha lakini hakuna hata mmoja aliyekubali kufikia hatua ya kufunga naye pingu za maisha. Amesema wengi walidai kuwa hawako tayari kiuchumi kutokana na ukosefu wa ajira pamoja na misukosuko ya kiuchumi nchini humo.

Tony Nweje, mwanaume mwenye umri wa miaka 44 ambaye hajaoa alipoulizwa, alieleza pia kuwa anatamani kufunga ndoa na kuwa na familia lakini kutokana na kutokuwa na kazi nzuri pamoja na maisha yanayoridhisha anaogopa kuwa mazao ya ndoa hiyo hataweza kuyamudu.

Uchenna Udogu mwenye umri wa miaka 40, yeye amekaririwa kuwa alidai kuwa hataki kufunga ndoa kwakuwa hataki usumbufu kwenye maisha yake.

“Wote tunafahamu kinachotokea kati ya wana ndoa katika familia nyingi hasa pale ambapo baba hana fedha. Hakuna mwanaume timamu anayetaka kuingiza kichwa chake kwenye hali kama hiyo,” alisema Udogu.

Kutokana na hali hiyo, mwanasheria maarufu mwanamke jijini Lagos, Barrister Sherry Osakwe alieleza kuwa endapo Serikali ya nchi hiyo haitaongeza jitihada za kutoa ajira na kuongeza kipato cha wananchi wake, wataathiri ndoto za kijamii za wanawake wengi wenye umri zaidi ya miaka 35 na kupunguza idadi ya familia zenye maisha ya ndoa yenye afya.

Wataalam wa masuala ya uhusiano wameeleza kuwa pamoja na mambo mengine, hali hiyo imesababishwa pia na mabadiliko makubwa ya maisha katika jamii, hususan kuanzishwa kwa mahusiano ya kimapenzi yasiyo rasmi yanayochukuliwa kama mahusiano rasmi katika jamii. Hivyo, hatua ya ndoa inapoteza maana kwa vijana wenye uelewa mdogo.

Mtazamo wa mhariri:

Vijana, tukumbuke kuwa ndoa ni jambo jema tuliyopewa na mwenyezi Mungu, uchumi isiwe kisingizio kwani sio sababu ya msingi wa ndoa tuliyopewa na Mungu.

Mithali 18:22 apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa Mungu.

JPM asema Changamoto zitakazoshindikana awamu hii hazitatatuliwa mbeleni
video: Mbowe augua ghafla mahabusu, CAG atoa msimamo

Comments

comments