Mabingwa wa soka nchini England Manchester City wamefanikiwa kumsajili kiungo mshambuliaji kutoka nchini Algeria Riyad Mahrez kwa ada ya Pauni milioni 60 akitokea Leicester City.

Mahrez amekamilisha usajili huo na kukubali kusaini mkataba wa miaka mitano ambao utamuweka Etihad Stadium hadi mwaka 2023, huku akichagua kutumia namba 23 katika jezi atakayoivaa msimu ujao klabuni hapo.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27, ametua Man City kwa pendekezo la meneja Pep Guardiola, ambaye alionyesha kuhitaji huduma yake tangu mwezi Januari mwaka huu, lakini taratibu za uhamisho wake zilikwama dakika chache kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.

Akizungumza mara baada ya kukamilisha usajili wake klabuni hapo Mahrez alisema: “Ninajihisi furaha kuwa sehemu ya klabu hii, nilitamani muda mrefu kufikia lengo hili, leo limetimia sina budi kumshukuru mwenyezi mungu pamoja na Pep Guardiola.

“Naamini ushirikiano nitakaouonyesha dhidi ya wachezaji wenzangu, tutafanikisha hatua kubwa ya kutetea taji la England, ambalo lilitua hapa msimu uliopita.”

Naye mkurugenzi wa soka wa Man City Txiki Begiristain alisema: “Riyad ni mchezaji wa kipekee, mwenye uwezo mkubwa wa kupambana, tunaamini atafanikisha malengo tuliyoyakususdia kuelekea msimu mpya wa ligi, tunamkaribisha kwa moyo mkunjufu.

Mahrez atakua na shughuli ya kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza cha Man City kwa kupambana na wenyeji Kevin De Bruyne, Raheem Sterling, David Silva, Leroy Sane na Bernardo Silva.

Tanzia: Mke wa Kibonde afariki dunia
Watoto 12 walionasa kwenye pango waokolewa, wafunguka

Comments

comments