Kiungo mshambuliaji wa klabu bingwa nchini England Leicester City Riyad Mahrez, amemaliza fununu za kuondoka klabuni hapo kwa kukubali kusaini mkataba mpya wa miaka minne ambao utamuweka King Power Stadium hadi mwaka 2020.

Arsenal ilikua moja ya klabu inayotajwa huenda ingemsajili kiungo huyo kutoka nchini Algeria, lakini mpango huo ulishindikana kutokana na msimamo uliokua umewekwa na meneja wa Leicester City Claudio Ranieri kwa kumshawishi Mahrez kubaki King Power Stadium.

Hata hivyo pamoja na mpango huo wa kusaini mkataba mpya kufanikiwa, bado Mahrez ana nafasi ya kuihama Leicester City mwishoni mwa msimu huu, endapo klabu ambazo aliziainisha zitajitokeza na kuhitaji huduma yake.

Mahrez alikiri kutamani kucheza soka nchini Hispania katika klabu ambazo zina umaarufu mkubwa duniani FC Barcelona pamoja na Real Madrid.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25 alisajiliwa na Leicester City  mwezi januari mwaka 2014, na mwishoni mwa msimu uliopita alitangazwa kuwa mchezaji bora wa chama cha wachezaji wa kulipwa nchini England PFA.

Shughuli kubwa ya kuisaidia Leicester City  kwa msimu wa 2015/16 na kupelekea kutwaa ubingwa wa England ilichagiza kuchaguliwa kwake kwa kupigiwa kura na wachezaji wenzake wa ligi hiyo na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa PFA.

Mahrez alifunga mabao 17 na kutoa pasi 11 za mabao msimu uliopita, na katika mchezo wa ufunguzi wa msimu huu dhidi ya Hull City, uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita lifunga bao la kufutia machozi kwa upande wa Leicester City, ambao walikubali kibano cha mabao mawili kwa moja.

Mahrez anakuwa mchezaji wa pili wa Leicester City kuikataa klabu ya Arsenal katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi, akitanguliwa na Jamie Vardy ambaye alikataa kuelekea kaskazini mwa jijini London miezi miwili iliyopita licha ya ofa ya usajili wake kutumwa King Power Stadium.

Rais Magufuli ateua Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha
Emmanuel Mbasha azungumzia uwezekano wa kurudiana na Flora