Kiungo mshambuliaji Riyad Mahrez huenda akafanyiwa vipimo vya afya juma hili, baada ya uongozi wa klabu ya Leicester City kukubali ofa ya Pauni milioni 60 iliyotumwa na mabingwa wa soka nchini England Manchester City.

Harakati za kiungo huyo kuondoka klabu hapo na kuhamia kwa mabingwa wa England, zilianza kuonekana tangu mwanzoni mwa mwaka huu wakati wa dirisha dogo la usajili, lakini taratibu za uhamisho wake zilikwama siku ya mwisho.

Pamoja na hali hiyo, Mahrez aliwahi kuomba kuondoka klabuni hapo na kufikia hatua ya kugoma kufanya mazoezi na wachezaji wenzake, lakini uongozi uliendelea na msimamo wa kukataa harakati za uhamisho wake, kwa kutaka walipwe ada ya pauni milioni 90.

Mahrez, mwenye umri wa miaka 27, mwanzoni mwa juma hili alijumuika na wachezaji wenzake wa Leicester City, kuanza maandalizi ya msimu mpya wa ligi.

Endapo usajili wa Mahrez utafanikiwa, utaweka rekodi ya kuwa ghali zaidi katika historia ya klabu ya Leicester City.

Msigwa: Sifikirii kuwa Rais, lakini 2020 Chadema tunachukua nchi
Arsenal, Juventus kupata ahuweni kwa Steven N’Zonzi