Uongozi wa Simba SC umemkabidhi Kocha Mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ jukumu la kusimamia usajili wa timu hiyo pamoja na kukata majina ya wachezaji ambao hawapo kwenye mipango yake msimu ujao.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo, Salim Abdallah “Try Again’ baada ya kupokea ripoti kutoka kwa Mbrazili huyo inayoonesha upungufu wao wa msimu uliopita na sehemu za kuimarisha kuelekea msimu unaokuja.

Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa yeye na viongozi wenzake wameamua kushirikiana na Robertinho katika kusaka wachezaji ambao watakiimarisha kikosi chao na kuwafanya kuwa bora kama ilivyokuwa msimu minne iliyopita.

“Tumepanga kuanza na usajili ndio maana ndani humu tumemshirikisha kocha Robertinho lakini baada ya hapo tutaweka nguvu kwenye maandalizi ya kujiandaa na msimu mpya na michuano ya Super Ligi na mwisho kabisa ni kuondoa wachezaji ambao mchango wao ni mdogo ndani ya timu,” amesema Try Again.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa katika msimu huu timu yao haikuwa katika ubora ule ambao walitarajia hiyo ni kutokana na makosa waliyoyafanya hasa katika usajili sasa hawataki makosa hayo yajirudie msimu ujao, ndio maana wamekusudia kufanya usajili wa nguvu kwenye dirisha kubwa la usajili.

Amesema mbali ya mchakato huo wa usajili pia wameanza mazungumzo na baadhi ya wachezaji ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu na anaamini mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi wa sita wachezaji wote ambao kocha amehitaji kuendelea nao msimu ujao watakuwa wameshasaini mikataba mipya.

Baadhi ya wachezaji ambao huenda wasiwepo kwenye kikosi cha Simba cha msimu ujao kutokana na mchango mdogo kwenye timu hiyo ni Beno Kakolanya, Nassoro Kapama, Peter Banda, Jonas Mkude, Mohammed Outtara, Augustine Okrah, Jimsony Mwanuke, Israel Mwenda, Habibu Kyombo na Ismail Sawadogo.

Hivi karibuni Rais wa Heshima wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ alikaririwa akisema kuwa atashughulikia usajili wa timu hiyo ili kuhakikisha msimu ujao inawania mataji.

Wajiri watakiwa kujisajili, kuwasilisha michango WCF
Serikali kujenga Meli tatu mpya nyingine zikikarabatiwa