Baada ya kuvunja kambi kufuatia mabadiliko ya ratiba, kikosi cha Simba leo Jumatano (Mei 24) kimerejea kambini kuanza rasmi maandalizi ya michezo yao miwili ya mwisho, huku Kocha Mkuu Mbrazili Robert Olivieira akitenga siku tisa sawa na saa 216 kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Simba SC imesaliwa na michezo miwili ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania utakaopigwa Juni 6, mwaka huu kabla ya kumalizana na Coastal Union Juni 9, mwaka huu.

Mpaka sasa Simba SC ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na alama zao 67 walizokusanya kwenye michezo 28 waliyocheza wakishinda mechi 20, sare saba na kupoteza mchezo mmoja, tayari bingwa amepatikana ambaye ni Young Africans.

Robertinho amesema: “Kuendana na mabadiliko ya ratiba yetu kikosi sasa kimerejea kambini leo Jumatano, kwa ajili ya kuanza maandalizi ya michezo yetu miwili iliyosalia dhidi ya Polisi Tanzania na ule dhidi ya Coastal Union.

“Kama ambavyo nilisema awali kuwa kwa sasa tunapaswa kusahau changamoto tulizopitia msimu huu, na mawazo yetu yote ni katika kuhakikisha tunamaliza msimu kwa nguvu zaidi.”

Tanzania, Qatar kushirikiana uchimbaji wa Mafuta, Gesi
RC Kagera aahidi kusimamia fedha za miradi ya maendeleo