Aliyekua meneja wa Man City Roberto Mancini, amekiri kufurahishwa na uwezo wa kisoka wa mshambuliaji kutoka nchini Italia Mario Balotelli ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya Nice ya Ufaransa.

Mancini ambaye kwa sasa ahana kazi baada ya kuachana na Inter Milan mwanzoni mwa msimu huu, amesema uwezo wa mshambuliaji huyo umekua ukimpa faraja kila kukicha kutokana na kumfahamu vyema Balotelli tangu akiwa na umri mdogo.

Amesema mshambuliaji huyo alionyesha hajakomaa kiakili alipokua katika klabu za Inter Milan, Man City, AC Milan na Liverpool na wakati mwingine aliwakera waliokua karibu yake, lakini kwa upande wake aliamini ipo siku Balotelli atakua, na kuthibitisha uwezo wa kisoka kwa vitendo.

“Yupo sawa kiumri na mwanangu wa kiume, na nilimlea kama mwanangu tangu tulipokua Inter Milan na nilijitahidi kumsajili nilipokwenda Man City na yote yaliyotokea Etihad Stadium yalichangiwa na ujana ulikua unamsumbua.

“Kijana mdogo hawezi kuendelea kufanya mambo ya kitoto kila siku, hufikia wakati anabadilika na ndivyo ilivyo kwa Balotelli, binafsi ananifurahisha na kunifariji kila ninapomuangalia akicheza katika ligi ya Ufaransa.

“Nina matumaini makubwa na Balotelli, kutokana na ushindani uliopo katika ligi ya Ufaransa, atabadilika zaidi ya ilivyo sasa.

“Wachezaji kama Balotelli wapo wachache sana duniani, na ni vigumu kukaa nao na kuwavumilia, lakini mimi niliweza kufanya hivyo japo ilinilazimu kumuondoa Man City.” Alisema Mancini alipofanyiwa mahojiano maalum na kituo cha Sky Sport Italia.

Mancini aliwahi kumkunja Balotelli alipokua Man city kutokana na nidhamu mbovu aliyokua nayo, lakini baadae alitangaza kumsamehe.

Video: Makonda atoa maamuzi mazito kuhusu Machinga Dar
Wenger Awavuruga FC Barcelona, Waanza Kumfikiria Glen Johnson