Mashabiki wa soka nchini Ubelgiji wametumia nafasi yao ya ushangiliaji kwa kumzomea kocha mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo Roberto Martinez, wakati wa mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Hispania uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo.

Mchezo huo ambao ulimalizika kwa kikosi cha Ubelgiji kukubali kufungwa mabao mawili kwa sifuri, ulikua wa kwanza kwa kocha huyo tangu alipokabidhiwa majukumu na chama cha soka nchini humo kama mbadala wa Marc Robert Wilmots.

Mabao ya Hispania katika mchezo huo yalifungwa na David Silva, na yalionekana kuwakera mashabiki wa Ubelgiji na kufikia hatua ya kumzomea Martinez kama ishara ya kutoikubali kazi yake.

Martinez ambaye alitimuliwa na uongozi wa Everton miezi miwili iliyopita kufuatia mwenendo wa kikosi cha klabu hiyo kwa msimu uliopita, amekua akipata changamoto za kukubalika miongoni mwa mashabiki wa Ubelgiji tangu alipotangazwa kuwa kocha mkuu.

Ubelgiji wameutumia mchezo wa Hispania kama kipimo cha kuelekea katika mpambano wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, ambapo mwanzoni mwa juma lijalo watawakabili Cyprus katika dimba la GSP mjini Nicosia.

Wakati huo huo ushindi wa Hispania katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Ubelgiji, umekua wa kwanza kwa kocha mpya wa timu hiyo Julen Lopetegui ambaye amechukua nafasi ya Vicente del Bosque aliyetangaza kujiuzulu mara baada ya fainali za Euro 2016.

Video: DC Mjema akabidhi daipa elfu 85,000 Hospitali ya Amana DSM
Samir Nasri: Ni Maamuzi Yangu, Pep Guardiola Hapaswi Kulaumiwa