Mshambulaiji wa klabu ya Feyenoord Rotterdam ya Uholanzi Robin van Persie amewahakikishia mashabiki wake, ataendelea kucheza soka angalau kwa msimu mmoja zaidi.

Van Persie ametoa uhakika huo, baada ya kuisaidia Feyenoord Rotterdam kutwaa ubingwa wa kombe la Uholanzi (Dutch Cup) mwezi uliopita, jambo ambalo lilionekana kumpa faraja kubwa kutokana na mapenzi alionayo dhidi ya klabu hiyo iliyomkuza kabla ya kutimkia Arsenal mwaka 2004.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 34, alifunga moja ya mabao yaliyoipa ushindi wa mabao matatu kwa sifuri Feyenoord, katika mchezo wa fainali ya kombe la Uholanzi dhidi ya AZ Alkmaar mwezi uliopita.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maamuzi alioyachukua, Van Persie ambaye ameitumikia timu ya taifa ya Uholazni katika michezo 102 na kufunga mabao 50, amesema amedhamiria kuendelea kubakia klabuni hapo kwa msimu mmoja zaidi.

Amesema kutokana na hatua hiyo, anatarajia kusaini mkataba mpya wakati wowote kuanzia sasa, na anaamini msimu ujao wa ligi atasaidiana na wengine ili kufanikisha mpango wa kutwaa ubingwa wa ligi ya Uholanzi.

“Nitaendelea kucheza hapa, bado nina nguvu na uwezo wa kufanya hivyo kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu,” amesema.

“Naamini watu wengi watakua wameshtushwa na maamuzi haya, lakini niwatoe hofu kwa kuwaambia kuwa, bado ni nguvu za kutosha na uwezo wa kufunga mabao kama ilivyo sasa.”

Klabu ya Feyenoord Rotterdam ilimsajili Van Parsie wakati wa dirisha dogo la usajili (mwezi Januari mwaka 2018) akitokea nchini Uturuki alipokua akiitumikia klabu ya Fenerbahçe.

Video: Rais Magufuli afichua madudu bandari kuu Dar
11 waliocheza 2014 waitwa kikosini Ureno