Aliyekua mshambuliaji wa klabu za Arsenal na Manchester United zote za nchini England Robin van Persie, amethibitisha kustaafu soka itakapofika mwishoni mwa msimu huu.

Van Persie, mwenye umri wa miaka 35, ametangaza maamuzi hayo akiwa nchini kwao Uholanzi, ambapo kwa sasa anaitumikia klabu yake ya zamani Feyenoord, ambayo ilimkuza na baadae kumuuza kwa washika bunduki wa kaskazini mwa jijini London (Arsenal) mwaka 2002.

Mshambuliaji huyo amesema anaamini muda wa kufanya hivyo umewadia baada ya kuutumikia mchezo wa soka kwa muda mrefu, na kupata mafanikio akiwa na klabu tofauti, hali ambayo amesema ataendelea kujivunia katika maisha yake yaliyosalia hapa duniani.

“Lini unatarajia kuacha kucheza soka?” Ni swali alililulizwa mshambuliaji huyo na waandishi wa habari nchini Uholanzi,  na kisha alijibu: “Ninatarajia kuachana na mchezo huu mwishoni mwa msimu huu, itakua ni upande wa kucheza pekee yake, lakini nitaendelea kuwa sehemu ya mchezo huu katika sekta nyingine.”

“Mwaka ujao nitafikisha umri wa miaka 36, nitakua ninatimiza muda wa miaka 18 wa kucheza soka langu katika kiwango cha kimataifa, sina budi kujipongeza kwa hili, maana ilikua ni ndoto yangu kwa muda mrefu.”

“Nilipokua na umri wa miaka mitano nilijiwekea malengo ya kucheza soka katika nchi mbalimbali barani Ulaya, namshukuru mungu dhamira  imetimia, na ninatangaza kuacha kucheza soka nikiwa katika ardhi ya nyumbani Uholanzi.”

Kwa upande wa timu ya taifa ya wakubwa ya Uholanzi, Van Persie alifanikiwa kufunga mabao 50 katika michezo 102 aliyocheza tangu alipoitwa kwa mara ya kwanza 2004.

Kabla ya hapo aliwahi kucheza katika timu za taifa za vijana Uholanzi: mwaka 2000 – kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 17, michezo 6 hakufunga bao, mwaka 2001 kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 19, michezo 6 hakufunga bao, na mwaka 2002–2005 kikosi cha umri wa miaka 21, michezo 12 alifunga bao moja.

Van Persie alikua sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Uholanzi kilichoshoriki fainali za kombe la dunia mwaka 2010 na kuishia nafasi ya pili baada ya kufungwa na Hispania bao moja kwa sifuri, mwaka 2014 aliiwezesha timu hiyo kuchukua medali ya mshindi wa tatu.

Mafanikio mengine aliyoyapata katika medani ya soka, ni kutwaa ubingwa wa UEFA Cup akiwa na Feyenoord mwaka 2002.

Akiwa na klabu ya Arsenal, Van Parsie alicheza soka chini ya aliyekua meneja klabuni hapo Arsene Wenger kwa muda wa miaka minane, huku akifunga mabao 132 katika michezo 278.

Alijiunga na Man Utd mwaka 2012 kwa ada ya Pauni milioni 24 na alikua chaguo la kwanza la aliyekua meneja wa klabu hiyo Alex Ferguson, na katika msimu wake wa kwanza alifanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi ya England, huku akiwa mfungaji bora na baadae kutangazwa kuwa mchezaji bora wa tuzo ya chama cha wachezaji wa kulipwa PFA.

Aliendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Man Utd chini ya utawala wa meneja David Moyes na baadae Louis van Gaal, lakini mwaka 2015 aliuzwa na kujiunga na klabu ya Fenerbahce ya Uturuki, mwaka 2017 alirejea nyumbani kwao Uholanzi baada ya kusajiliwa na Feyenoord, ambayo aliisaidia kutwaa ubingwa wa kombe la Uholanzi (Dutch cup) msimu uliopita.

Zitto aishukia serikali kuhusu Trilioni 1
Video: CCM yazungumzia kutekwa Mo Dewji, Waziri ashusha rungu ajali magari serikalini