Aliyekua meneja wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers, amewashukuru wachezaji pamoja na mashabiki wa klabu hiyo kwa ushirikiano mkubwa waliomuonyesha wakati wote alipokua kazini tangu mwaka 2012.

Rodgers, amewasilisha salamu hizo za shukurani kwa njia ya tovuti ya chama cha mameneja wa soka nchini England, ambapo ameeleza kufurahishwa na mazuri yote aliyoyafanya kwa ushirikano wa kila mmoja klabuni hapo.

Meneja huyo kutoka Ireland ya kaslazini, ameeleza kuendelea kuifuatilia klabu hiyo kutokana na mazuri aliyoyaacha huko Anfield na pia ameahidi kuiombea dua njema, ili iweze kufikia malengo yanayokusudiwa na viongozi wake.

Rodgers, pia ameeleza masikitiko yake ya kuondolewa kazini mara baada ya mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita ambapo alilazimishwa sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Everton, kwa kubainisha imekua kama bahati mbaya kwake kutokana na kushindwa kufikia mipango aliyokua amejiwekea tangu alipoajiriwa mwaka 2012.

Amesema ni vigumu kueleza yaliyo moyoni mwake, lakini hana budi kukubaliana na hali halisi ambayo imekua ikiwatokea mameneja wa soka duniani kote hususana linapofika suala la kufutwa kazi.

Hata hivyo Rodgers amesisitiza suala la kupumzika kwa sasa, na kama atapata kibarua kingine katika kipindi hiki kifupi, atakua tayari kurejea kazini kutokana na kuhitaji kufanya hivyo kufuatia mapenzi aliyonayo katika mchezo wa soka.

Wakati huo huo chama cha mameneja nchini England kimetoa tamko la kutikitishwa na hatua ya kutimuliwa kwa Rodgers, kwa kusisitiza bado kulikua na nafasi kuaminiwa kwa mtu huyo, kutokana na mazingira ya kazi yake ambayo hayakua mabaya tangu mwanzoni mwa msimu huu.

 

Jose Mourinho Aharibu Tena FA
Bale Atawala Kwa Ubora Nchini Wales