Kiungo mshambuliaji kutoka nchini Colombia James David Rodríguez Rubio, amejiunga na klabu ya Everton ya England, akitokea kwa mabingwa wa Hispania Real Madrid.

Kiungo huyo ameondoka Santiago Bernabeu, kufuatia changamoto ya kukosa nafasi ya kuchezea kwenye kikosi cha kwanza cha meneja wa mabingwa hao wa La Liga Zinedine Zidane kwa kipindi kirefu, hali ambayo ilimfanya apelekwe kwa mkopo kwenye klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani, kuanzia mwaka 2017–2019.

Meneja wa Everton Carlo Ancelotti ambaye amewahi kufanya kazi na kiungo huyo alipokua mkuu wa benchi la ufundi la Real Madrid, amefanikisha usajili wa Rodrigues, huku akimini uwepo wake kwenye ligi ya England kuanzia msimu ujao, utafanikisha kurejesha makali ya nahodha huyo wa timu ya taifa ya Colombia.

Baada ya kukamilisha mpango wa kujiunga na The Toffees kwa mkataba wa miaka miwili, Rodriguez alizungumza na Televisheni ya klabu ya Everton na kusema: “Ninafuraha sana kujiunga na Everton, klabu yenye historia kubwa na meneja anayenifahamu vizuri.”

“Ninatarajia kubeba mataji nikiwa na klabu hii, hiki ni kitu ambacho kila mtu anakitegemea. Nimekuja hapa kujiendeleza na kuisaidia timu kupata ushindi na kucheza soka safi.”

“Nimeshawishika na Carlo pamoja na benchi lake la ufundi, tutaweza kupata mafanikio. Yeye ndio sababu kubwa ya mimi kujiunga na timu hii. Nimefurahia nyakati zote nilizofanya nae kazi katika vilabu viwili tofauti.”

“James kama kila mtu anavyomjua, ni mchezaji mzuri, anakiwango na anaweza kutoa pasi za magoli kwa washambuliaji. Alivutiwa na tunachokifanya na sikutumia muda mwingi kumshawishi kujiunga nasi kwa sababu alikuwa tayari ameshavutiwa na tunachokifanya” amesema Carlo Ancelotti.

Rodriguez anaondoka Real Madrid huku akiacha historia ya kucheza michezo 89 na kufunga mabao 25 tangu alipoanza kuitumikia klabu hiyo mwaka 2014, aliposajiliwa akitokea AS Monaco ya Ufaransa.

TMA: Pandeni mbegu za muda mfupi
Vifahamu vipaumbele vya CUF kuelekea uchaguzi mkuu