Mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji Romelu Menama Lukaku Bolingoli hatokua sehemu ya kikosi cha Man Utd kitakacho pambana hii leo katika mchezo wa mkondo wanne wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, hatua ya makundi dhidi ya mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC.

Meneja wa Man Utd Jose Mourinho amethibitisha taarifa za mshambuliaji huyo kutokua sehemu ya kikosi chake baadae hii leo, na pia amesema yupo kwenye hati hati ya kucheza mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England dhidi ya Man City, mwishoni mwa juma hili.

Lukaku, ambaye mpaka sasa ameshaifungia Man Utd mabao manne huku mara ya mwisho akifunga katikati ya mwezi Septemba, alikosa mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Bournemouth, kufuatia majeraha ya misuli ya paja yanayomkabili.

“Lukaku hatokua sehemu ya mchezo wetu dhidi ya Juventus FC, na tuna mashaka ya kumtumia katika mchezo wa mwishoni mwa juma hili dhidi ya Man City,” alisema Mourinho akiwa katika mkutano na waandishi wa habari mjini Turin.

Katika hatua nyingine Mourinho akazungumzia mchezo wa leo, kwa kusema utakua na hali ya ushindani mkubwa, hasa baada ya kikosi chake kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza majuma mawili yaliyopita, ambapo ilishuhudiwa Juventus wakiibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri kwenye uwanja wa Old Trafford.

“Tumeyafanyia kazi mapungufu yaliyosababisha tukapoteza mchezo uliopita, ninaamini tutapambana kivingine tofauti na ilivyokua Old Trafford, kwa mantiki hiyo ninaamini mchezo utakua mgumu kwa kila upande”

“Ninaamini mpira wa miguu jibu lake kamili hupatikana baada ya dakika 90, mengi kwa sasa yanazungumzwa hususan upande wa mashabiki, kila mmoja anazungumza lake, lakini uhalisia wa mambo yote yataonekana uwanjani, na timu iliyojiandaa vyema itapata matokeo mazuri.”

Kivutio kikubwa katika mchezo wa leo ni mshambuliaji wa Juventus Cristiano Ronaldo kucheza kwa mara ya kwanza na klabu yake ya zamani kwenye uwanja wa Juventus Stadium, huku aliyekua kiungo wa mabingwa hao wa Italia Paul Pogba, akitarajiwa kurejea kwa mara ya kwanza mjini Turin, baada ya kuondoka misimu miwili iliyopita.

Juventus wanaendelea kuondoka msiamamo wa kundi H kwa kufikisha alama tisa, huku Man Utd wakifuatia katika nafasi ya pili kwa kumiliki alama nne, na Valancia wapo nafasi ya tatu kwa kuwa na alama mbili. Young Boys kutoka Uholanzi inaburuza mkia wa kundi hilo kwa kumiliki alama moja.

Marais wanne wa zamani wachuana tena Madagascar
Wahuu afunguka kuhusu majuto baada ya kuingia kwenye muziki wa injili