Mchezaji wa klabu ya Juventus ya nchini Italia, Cristiano Ronaldo amekanusha vikali tuhuma za ubakaji zilizoelekezwa kwake na mwanamke mmoja raia wa Marekani, aliyedai kuwa alimbaka mwaka 2009.

Katika tuhuma hizo, Kathryn Mayorga anadai kuwa Ronaldo alimbaka kwenye chumba cha hoteli moja jijini Las Vegas.

Ronaldo ametumia akaunti yake ya Instagram kueleza kuwa habari hizo ni za uongo na kwamba wanaofanya hivyo wanataka kutumia jina lake.

“Wanataka kutumia jina langu ili wajitangaze, hiyo ni kawaida,” amesema Ronaldo.

Mwanasheria wa Ronaldo, Christian Schertz amesema kuwa watalishtaki jarida la Ujerumani la Der Spiegel ambalo lilikuwa la kwanza kuchapisha tuhuma hizo.

Schertz amesema kuwa kitendo cha jarida hilo kuchapisha tuhuma hizo ni shambulio lililo kinyume cha sheria. Amesema kuwa amepewa maelekezo ya kufungua kesi dhidi ya jarida hilo kudai fidia ya kuchafua jina la Ronaldo.

Aidha, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 34 anadaiwa kufungua faili la tuhuma za ubakaji katika kituo cha polisi cha Las Vegas.

 Katika faili hilo, mwanamke huyo anadai kuwa Ronaldo na timu yake waliwahi kumtafuta mwaka 2010 na kuahidi kumlipa $375,000 ili asipeleke kesi hiyo mahakamani au hata kuisema hadharani.

Hivyo, mwanasheria wa mwanamke huyo anadaiwa kufanya jitihada za kuomba mahakama kubatilisha makubaliano hayo ya usiri ya mwaka 2010.

Hii ni changamoto ya kwanza kubwa nje ya uwanja dhidi ya Ronaldo tangu alipojiunga na Juventus akitokea Real Madrid kwa dau la zaidi ya   £99.2 Milioni.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Oktoba 1, 2018
CCM yatoa karipio kwa wanaotafuta Urais Zanzibar

Comments

comments