Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya nje, Bernard Membe amemjibu mbunge wa zamani wa Igunga, Rostam Aziz kuhusu sakata la kutaka kukivuruga Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwania tiketi ya kugombea katika uchaguzi ujao.

Hivi karibuni, Rostam aliwaambia waandishi wa habari kuwa Membe anapaswa kuzingatia utamaduni wa CCM wa kupeana awamu mbili, na kwamba awamu ya kwanza huchukuliwa kama dakika 45 za kipindi cha kwanza cha mechi ya mpira wa miguu kitakachokamilika baada ya miaka kumi kutimiza dakika 90.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, Membe amesema kuwa anamshauri Rostam kujikita katika kuzungumzia masuala ya kitaifa yanayohusu uchumi kwani yeye ni mchumi.

Alieleza kuwa yeye na mfanyabiashara huyo wote wana hali moja ndani ya chama hicho akidai kuwa wote wamekatwa mikia na ni watoto wa kambo.

“Anafanya vizuri anapojihusisha na masuala ya uchumi na asijaribu kuwa more Christian than the Romans (kuwa mkristo zaidi ya Warumi). Rostam wewe ni mwenzetu sisi, tumekatwa mikia au sio jamani. Tumeshakatwa mikia, hata ukijitahidije mkia wako ni mfupi tu,” amesema Membe.

“Na tunayoyazungumza ni vizuri tuwe consistent (na muendelezo). Tunayoyazungumza kwenye dhamira yetu na tunayoyazungumza mdomoni. Tuwe tunazungumza kitu ambacho binadamu wanatuheshimu; na namshauri tena Rostam, ni mchumi mzuri sana, tuzungumzie masuala ya uchumi wa nchi yetu. Haya yatampa heshima kubwa kuliko kujaribu kuwa mtoto mzawa badala ya kukubali status ya kwamba Rostam na mimi ni watoto wa kambo,” ameongeza.

Membe amekuwa akitajwa kuwa anafanya vikao na kuanza kampeni ya mapema ya chinichini akitaka kuchukua fomu ya kugombea kupitia CCM mwaka ujao. Hali hiyo imekuwa ikiambatana na hisia kuwa kuna nia mbaya ya kutaka kukigawa chama hicho bila kufuata utaratibu wa chama.

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally aliwahi kutangaza kumuita Membe ofisini kwake ili ajieleze kuhusu taarifa hizo.

Membe: Rostam wewe ni mwenzetu, wote ni watoto wa kambo
Shirikianeni katika kazi, vinginevyo nitawang'oa wote- JPM