Aliyekua kocha mkuu wa timu ya taifa ya England Roy Hodgson ametangaza kuwa mbioni kurejea katika utawala wa soka, baada ya kukaa pembeni za zaidi ya miezi minne.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 69, amekua nje ya tasnia ya ukufunzi wa soka, kufuatia kujizulu nafasi ya ukocha mkuu wa timu ya taifa ya England siku chache baada ya The Three Lions kutupwa nje ya michuano ya Euro 2016 kwa kufungwa na Iceland mabao mawili kwa moja.

Hodgson amesema anaamini muda aliokaa nje ya shughuli ya ukufunzi wa soka unatosha, na amejifunza mambo mengi ambayo anaamini atakaporejea atayafanyia kazi kwa ufanisi mkubwa.

“Ninajipanga kurejea – ninajihisi vizuri zaidi kuliko nilivyokua. Kuhusu umri wangu sio tatizo kwa sababu naamini nilipofikia kwa sasa nimekomaa kwa kila hali,” Alisema Hodgson alipohojiwa na Sky Sports News.

“Ninaamini kila jambo litakaa sawa nitakaporejea katika majukumu ya ukocha – jambo kubwa kwa yoyote ambaye atakua tayari kufanya kazi na mimi ni uwepo wa uhuru kati yangu na yake pia.

“Ninasubiri ili kujua ni nani ambaye atakua wa kwanza kuzungumza na mimi ili tufanye kazi kwa pamoja, nipo tayari kurudi kwenye mapambano.” Aliongeza Hodgson

Kabla ya kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya England mwaka 2012, Hodgson aliwahi kuwa mkuu wa benchi la ufundi la klabu za Fulham (2010–2011), Liverpool, (2011–2012) na West Bromwich Albion (2012–2016).

Hodgson pia amewahi kuwa meneja wa baadhi ya klabu za nje ya England.

Gianni Infantino Akomaa Na Timu 48 Kombe La Dunia
Europa League Kumtega Jose Mourinho?