Nguli wa soka na aliyekuwa nahodha wa Manchester United Roy Keane, amefunguka kuwa hakuna timu yoyote kati ya timu yake ya zamani na Arsenal yenye uwezo wa kuingia ndani ya nne bora msimu huu.

Keane amesema hayo baada ya kutoridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na klabu hizo zilipokutana katika mchezo wa Ligi kuu nchini uingereza siku ya Jumatatu ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 katika dimba la Old Trafford.

Ilichukua dakika 28 ndipo shuti la kwanza langoni likapatikana katika mchezo huo, ikiwa ni rekodi ya shuti lililochelewa zaidi msimu huu katika mechi zote za ligi hiyo.

Kiungo Scott McTominay, aliifungia United bao la kuongoza sekunde chache kabla ya mapumziko, lakini PierreEmerick Aubameyang alisawazisha kipindi cha pili baada ya VAR kutengua maamuzi mabovu ya mwamuzi wa pembeni aliyedai straika huyo aliotea.

“Tumekuwa tukiangalia mechi za Manchester United na Arsenal na hatuamini jinsi mchezo huu ulivyokuwa mbaya,” alisema kiungo huyo wa zamani wa Manchester United.

“Kulikuwa na upungufu wa ubora, wachezaji walionekana kuwa chini ya kiwango, kadi za njano nyingi, hakukuwa na nidhamu. Lakini upungufu wa ubora unatisha, hakika.”

Nahodha huyo wa zamani wa Manchester United anaamini kuwa timu zote hizo mbili zitafanya kazi ya ziada  kuingia ndani kwenye nne bora na kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Alipoulizwa timu ipi itafanikiwa kumpiku mwenzake, Keane alijibu “Kwa kiwango cha usiku huu (juzi) hakuna itakayoingia.

“United wanatakiwa kuwekeza lakini ukiangalia kiwango cha usiku huu, West Ham na Leicester ndizo zitakazoingia.”

Lakini beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher, yeye amesema Arsenal itaingia nne bora kutokana na utajiri ilionao katika safu ya ushambuliaji.

“Nasema Arsenal kwa sababu watapata mabao mengi kupitia kwa Lacazette na Aubameyang,” alisema Carragher wakati akiuchambua mchezo huo.

Trump awawakia wabunge, adai kuna mtu anampeleleza Ikulu
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 3, 2019