Gwiji wa klabu ya Man Utd Roy Keane amemponda meneja wa sasa wa klabu hiyo Jose Mourinho na kumsifia mkuu wa benchi la ufundi la Man City Pep Guardiola.

Kean ambaye alicheza nafasi ya kiungo wakati wa utawala wa Sir Alex Ferguson ameibuka na kumponda Mourinho bila kusita kwa kusema meneja huyo hana hadhi ya kujiita “The Special One (Wa Kipekee)” na badala yake anaamini Guardiola ndio mwenye sifa hiyo.

Kean ameyazungumza maneno hayo alipohojiwa na kituo cha televisheni cha ITV cha nchini England, ambapo alitakiwa kueleza matarajio yake kuhusu Man Utd ambayo imeonyesha kukosa muelekeo tangu alipoondoka Sir Alex Ferguson sambamba na kusema machache juu ya Man City ambayo ipo chini ya meneja kutoka nchini Hispania Pep Guardiola.

Kean amesema haoni jipya ambalo litalojitokeza Old Trafford katika kipindi hiki ambacho Mourinho amekabidhiwa majukumu ya kukiongoza kikosi cha Man Utd, na kama itatokea itakua ni kama bahati.

Amesema Mourinho mara kadhaa amekua akiendesha soka kwa kubebwa na bahati na jambo hilo lilijidhihirisha wakati wa msimu uliopita alipokua na kikosi cha Chelsea ambapo alionekana kushindwa kazi na hatimae kutimuliwa.

Kwa upande wa Man City, Keane amesema ana matarajio makubwa na klabu hiyo kufanya vyema kwa msimu huu kutokana na kuonyesha umakini wa kumuajiria meneja ambaye amekuja na mtazamo tofauti wa ufundishaji soka.

“Guardiola ni mtu ambaye anaweza kufanya maamuzi yanayoleta tija na wakati mwingine mashabiki hushangazwa na hilo, lakini mwishoni mwa msimu mambo huwa mazuri kwa upande wake, hivyo natarajia makubwa kutoka kwa Man City kwa msimu huu,”

“Kuna baadhi ya mambo ameshayafanya mpaka sasa ndani ya kikosi cha Man City kwa kuwatoa baadhi ya wachezaji kwa mkopo na hatua ya kumuweka pembeni Yaya Toure kwenye orodha yake ya michezo ya Ulaya, ni jambo ambalo hata mimi lilinistaajabisha, lakini matokeo yake yameanza kuonekana, hasa baada ya timu kushinda mabao manne kwa sifuri usiku wa kuamkia hii leo dhidi ya Borussia Moenchengladbach,”

“Kutokana na mtazamo huo, ninaamini Guardiola anapaswa kupewa sifa ya kuitwa The Special One (Wa Kipekee), lakini sio Mourinho ambaye ameonyesha kupoteza muelekeo.” Alisema Kean

Kean amemponda Mourinho huku mashabiki wa Man utd wakiwa bado hawajasahau kichapo cha mabao mawili kwa moja walichokipokea kutoka kwa Man City mwishoni mwa juma lililopita.

Mchezo huo ulikua wa kwanza kwa msimu huu kuwakutanisha Mourinho na Guardiola tangu walipokutana kwa mara mwisho katika ligi ya nchini Hispania.

Video: Prof. Baregu apinga ripoti ya Twaweza, asema JPM anaminya demokrasia
Antonio Conte Kumkabidhi Gwanda David Luiz