WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ana nia thabiti ya kuwatumikia Watanzania na kuendelea kuleta maendeleo nchini kote hususani maeneo ya vijijini.
 
Amesema kuwa Serikali inapeleka miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, elimu na afya.
 
Ameyasema hayo leo (Jumanne, Novemba 23, 2021) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Lipande, Narungombe, Machang’anja na Namgurugayi akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Ruangwa.
 
Akizungumza baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa daraja la Mto Mbwemkuru linalounganisha wilaya ya Ruangwa na Liwale wenye thamani ya shilingi bilioni nne amesema mradi huo utapunguza adha ya usafiri katika maeneo hayo.
 
“Awali wananchi wa maeneo hayo walikuwa wanapata adha kubwa hasa kipindi cha masika ambapo walitumia mitumbwi na madumu kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine.”
 
Naye, Meneja wa TARURA wilaya ya Ruangwa Mhandisi Mashaka Nalupi amesema mradi huo ulianza kujengwa Januari 31, 2020 na unatarajiwa kukamilika Desemba 31, 2021 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 54.
 
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amezengumza na wananchi wa kata Narungombe baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha Afya cha kata hiyo, ambapo amesema ameridhishwa na ubora wake kwani umeendana na thamani ya fedha iliyoyolewa.
 
“Msisitizo wa mheshimiws Rais Samia kwenye ujenzi wa miradi ya Serikali ni ubora, kamati zote zilizopewa mamlaka ya kusimamia miradi hii ni lazima wajiridhishe na viwango vya ubora wake ili iendane na thamani ya fedha zilizotoka”
 
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kutofanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji. “Lindeni vyanzo vyetu vya maji, msiruhusu watu walime kwenye vyanzo kuweni walinzi wa maeneo hayo.”

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Novemba 25, 2021
Rais Samia aja na suluhu ajali za barabarani