Klabu za soka nchini Italia zimepewa tuhusa ya kuanza kufanya mazoezi ya pamoja kuanzia mwanzoni mwa juma lijalo (Mei 18), kabla ya kuanza rasmi kwa ligi ya Serie A, na ligi nyingine nchini humo.

Shirikisho la soka nchini Italia FIGC limetoa taarifa hizo, kufuatia Serikali ya nchi hiyo kutangaza utaratibu wa klabu za michezo kurejea katika utaratibu wa kufanya mazoezi ya pamoja, kufuatia ahuweni ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Kabla ya agizo hilo la Serikali, wachezaji wa soka na michezo mingine nchini Italia walikua wakifanya mazoezi binafsi nyumbani kwa kuhofia kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona, ambayo ilikuwa juu nchini humo.

Ligi ya Italia (Serie A) ilisimamishwa Machi 9, na mpaka sasa serikali  haijatangaza muda maalum ya kuendelea kwa ligi hiyo, licha ya kuwepo kwa matarajio makubwa kwa wadau wa soka nchini humo.

Timu maalum ya utafiti ya kisayansi ambayo ipo chini ya Serikali, inaendelea kufanya utafiti wa kina, ili kujiridhisha hali halisi ya maambukizi ya virusi vya Corona, ambayo hata hivyo yameripotiwa kupungua kwa kiasi kikubwa.

Majibu ya timu hiyo yanatarajiwa kutumika kama nyenzo ya kutoa ruhusa kwa viongozi wa shirikisho la soka nchini Italia (FIGC), kuendelea na ligi ama kusitishwa kwa msimu huu.

Waziri wa afya nchini Italia Roberto Speranza na waziri wa michezo Vincenzo Spadafora, wamesema timu hiyo inaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Serikali na wana matumani makubwa ya kupata majibu sahihi ambayo yatatoa mwanga wa kuendelea ama kufutwa kwa msimu wa ligi.

Ligi ya Italia imesaliwa na mizunguuko 12 kabla ya kukamilishwa kwa msimu wa 2019/20, huku mabingwa watetezi Juventus wakiongoza msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya alama moja dhidi ya SSC Lazio wanaoshika nafasi ya pili.

Mvua Afrika Mashariki zaathiri watu zaidi ya milioni moja
Joan Laporta: Nitamrudisha Pep Guardiola