Kiungo wa klabu bingwa nchini Ufaransa PSG, Adrien Rabiot, amepewa ruhusa ya kuondoka jijini Paris na kwenda mjini Barcelona Hispania kujiunga na mabingwa wa La Liga FC Barcelona, endapo mazungumzo ya uhamisho wake yatapata baraka za pande zote mbili.

Kwa mujibu wa tovuti ya SPORT, Rabiot tayari ameshafanya makubaliano binafsi na uongozi wa FC Barcelona, lakini bado uongozi wa PSG haujaafikiana na klabu hiyo kuhusu ada ya uhamisho wa kiungo huyo ambayo inatajwa kufikia Euro milioni 40.

Taarifa nyingine zilizochapishwa na gazeti la Le Parisien la Ufaransa, zinaeleza kuwa uongozi wa PSG umebariki kuondoka kwa Rabiot japo ada yake inaendelea kuwa kikwazo, kufuatia agizo lililotolewa na meneja wao mpya Thomas Tuchel, ambaye amesisitiza kiungo huyo hayupo kwenye mipango yake.

Taarifa hizo zimeongeza kuwa, Tuchel amelazimika kutoa ruhusa ya kuondoka kwa Rabiot kutokana na kuamini endapo atabaki klabuni hapo, hatokua mwenye furaha, hasa baada ya hitaji lake la kutaka kuondoka kukataliwa.

Meneja huyo kutoka nchini Ujerumani ameona ni bora Rabiot akaondoka na nafasi yake kujazwa na mchezaji mwingine, ambaye atakua na furaha ya kuitumikia PSG, itakayokua na kazi ya kutetea ubingwa wa Ufaransa msimu wa 2018/19.

Mkataba wa Rabiot na PSG, unatarajia kufikia kikomo baada ya miezi kumi na mbili ijayo, na amekataa kusaini mkataba mpya.

Uongozi wa PSG umefikia hatua ya kubariki mchakato huo, kwa kuhofia huenda Rabiot akaondoka kama mchezaji huru mwishoni mwa msimu wa 2018/19, hivyo wanaamini kiasi kitakachopatikana katika biashara ya usajili wake, kitasaidia kufanya usajili wa mchezaji mwingine.

Rabiot raia wa Ufaransa alikuzwa na klabu ya PSG na kuanza kuitumikia timu ya vijana mwaka 2012-2014, na kuapandishwa kwenye kikosi cha wakubwa ambacho ameshakitumikia katika michezo 136 na kufunga mabao 11.

Mwaka 2013 aliuzwa kwa mkopo kwenye klabu ya Toulouse, na huko alicheza michezo 13 na kufunga bao moja.

Majaliwa aagiza maafisa ugani kuwezeshwa na kusimamiwa kikamilifu
Clement Sanga aenguliwa bodi ya ligi