Rais wa klabu bingwa nchini Ujerumani FC Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge, ameijia juu klabu ya Man Utd kufuatia sakata la kiungo Bastian Schweinsteiger, ambaye yu njiani kuachwa na meneja Jose Mourinho.

Schweinsteiger, alijiunga na klabu hiyo ya Old Trafford, wakati wa utawala wa meneja Louis Van Gaal na usajili wake ulitarajiwa kuwa na mambo makubwa kwenye kikosi cha mashetani wekundu lakini imekua tofauti.

Rais wa FC Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge, ameishutumu Man Utd kwa kushindwa kumtumia ipasavyo kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32 na kumsababishia kiwango chake kuporomoka.

Rummenigge, amesema wameumizwa na hatua ya Man Utd kushindwa kumtumia Schweinsteiger kama ilivyokua matarajio ya wengi, na mwishowe wanafikia hatua ya kumuweka kwenye orodha ya wachezaji ambao wataondoka kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili mwishoni mwa mwezi huu.

“Siamini kama Schweinsteiger ameshindwa kucheza soka akiwa na Man Utd, bali ninachokiona hapa ni kushindwa kutumiwa ipasavyo katika kikosi cha klabu hiyo kama watu wengi walivyokua wanatarajia. Rummenigge aliliambia gazeti la Bild.

“Jambo kama hilo halikuwahi kufikiriwa alipokua Bayern Munich, na ndio maana alionekana kung’ara wakati wote.” Aliongeza Rummenigge

Hata hivyo kiongozi huyo amemshauri Schweinsteiger kurejea Allianz Arena endapo atahitaji kufanya hivyo kutokana na kuamini kwamba, bado ana nafasi kubwa ya kuonyesha uwezo wake na kuisaidia klabu hiyo ambayo ilianza kumtumia tangu mwaka 2005 wakati wa utawala wa meneja kutoka nchini Ujerumani Felix Magath.

Video: Tamko la TECMN kuhusu taarifa ya Serikali ya kukata rufaa kesi ya kupinga ndoa za utotoni
Menez Apoteza Kipande Cha Nyama Ya Sikio