Mwenyekiti wa CHAUMA, Hashimu Rungwe amezungumzia wimbi la wanasiasa kuhama vyama vyao katika kipindi hiki kifupi akidai kuwa wanamaslahi binafsi.

Akizungumza hivi karibuni na Radio DW, Rungwe amesema kuwa wimbi hili haliwezi kutishia uhai wa vyama vya siasa nchini kwani ni suala la kidemokrasia na uhuru wa kikatiba, lakini linafifisha ushindani wa vyama vingi vya siasa.

Aliongeza kuwa watu wanaohama wana maslahi yao binafsi na kwamba hali hiyo inatokana na mengi ikiwa ni pamoja na kile alichokiita ‘njaa’.

“Ofcourse wale watu wana maslahi fulani, sio kwamba wanakwenda tu. Tukifuatilia nyuma orodha ya waliohama ni kubwa, kuna akina [David] Kafulila, akina [Patrobas] Katambi, wote na orodha ni kubwa na nadhani hata wale ambao wako kule CCM kindakindaki, wale CCM wenyewe wanasikitika, wanaona kwanini sisi tunanyimwa hizo nafasi,” alisema.

Katika hatua nyingine, Rungwe aliwatahadharisha wanasiasa wanaobaki kwenye vyama vyao hasa wapinzani kuwa hali ya kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao (2020) itakuwa ngumu tofauti na ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliopita.

“Siasa za mwaka 2020 zitakuwa ngumu sana. Watu waliobaki kwenye vyama vyao [vya upinzani] wategemee kuwa siasa zitakuwa ngumu mno.”

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni wa Wakili binafsi wa Mahakama Kuu, alisema kuwa yeye haogopi kinachoendelea kwenye ulingo wa siasa hivi sasa kwani chama chake kipo na kina wanachama, lakini ametahadharisha kuwa kuna hofu ya kufifishwa kwa uhuru wa kujieleza.

Katika kipindi cha hivi karibuni, baadhi ya wabunge na viongozi wa vyama vya upinzani walitangaza kuachana na vyama vyao na kujiunga na chama tawala CCM, wakieleza kuwa wameridhishwa na utendaji kazi wa Serikali y CCM inayoongozwa na Rais John Magufuli hivyo wanaona ni vyema wajiunge na chama hicho ili kuunga mkono juhudi za kuleta maendeleo.

Wengine, akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara walidai kuwa migogoro ya uongozi na kuminywa kwa demokrasia ndani ya Chadema ni chanzo cha wao kukikimbia chama hicho cha upinzani. Siku chache zilizopita, Julius Mtatiro aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama Cha Wananchi (CUF), alitangaza kuachana na chama hicho na kujiunga na CCM.

Waitara, Julius Kalanga (Monduli) ni miongoni mwa waliochana na Chadema na sasa watagombea tena kwa tiketi ya CCM katika majimbo yao.

IGP Sirro: Kwasasa moto wetu ni mkali
Bobi Wine apatikana akiwa hawezi kuzungumza wala kutembea